Waziri Mabula akutana na wahariri, aeleza mwelekeo mpya

KUANZIA sasa, taasisi ama mtu yeyote anayetaka kutwaa maeneo ya ardhi kwa uwekezaji wowote, lazima awe na pesa mkononi za kukabidhi ama kuwalipa wenye maeneo yao hapo kwa hapo ili kuondoa migogoro.

Ni kauli ya Angelina Mabula, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mbele ya wahariri wa vyombo vya habari nchini, katika semina iliyofanyika leo tarehe 4 Juni 2022, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mabula amesema, wizara hiyo sasa imeunganishwa kutoka mfumo wa analogia kwenda kidigitali ili kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi.

“Sekta ya ardhi imeendelea kuwa kiunganishi kutoa analogia kwenda kidigitali, mikoa 25 na halmashauri 40 zimeunganishwa kidigitali ili kukabiliana na migogoro.

“Mfumo huu wa kidigitali kwanza utaondoa urasimu wakati wa upatikanaji hati, utaondoa pandikizi (kuuziana viwanja mara mbili mbili) pia utapunguza migogoro,” amesema Waziri Mabula.

Amewaeleza wahariri kwamba, wizara hiyo ikibaki nyuma kwenye maendeleo ya TEHAMA katika kuandaa maeneo, inaweza kukwamisha maeneo mengine ikiwemo uwekezaji.

Katika kukabiliana na migogoro ya ardhi, Waziri Mabula ameshauri wananchi wanaponunua viwanja, kabla ya kujenga, wakajiridhishe kwenye halmashaur zao.

“Ukitaka kujenga, baada ya kununua eneo, nenda halmashauri ukajiridhishe, vinginevyo ukienda kichwa kichwa ukajenga, mahakama ikionesha eneo lina umiliki, huna pa kukimbilia. Usijenge bila kujiridhisha, nenda halmashauri ,” amesema Waziri

Mabula na kuongeza;

 

“Tumeelekeza kuanzishwa kwa kliniki ya ardhi katika maeneo yote ili watu wenye matatizo yao wakutane nao mtaani, wasisubiri wawafuate ama kiongozi akiwa ziarani ndio waseme migogoro yao.”

Waziri Mabula ameeleza umuhimu wa vyombo ya habari nchini, kwamba vikisimama kutoa habari, nchi nayo itasimama.

“Vyombo vya habari vikisimama, vikaacha kutoa habari, nchi itakuwa kama imesimama. Hatuwezi kujua nini kinaendelea,” amesema.

Kwenye semina hiyo, Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amesema, Wizara ya Ardhi inagusa maisha ya Watanzania na ni chemchem ya migogoro.

Hata hivyo, Waziri Mabula amesema, wao wanasimamia sera na sheria na kwamba, kuna wengine wanaohusika katika mipango miji ingawa lawama zote zinapelekwa wizarani.

Allan Kijazi, Katibu Mkuu wa wizara hiyo amesema, wenye uwezo walikuwa wakitumia uwezo wao kuwakandamiza wanyonge.

Amesema, mfumo wa kidigitali unakwenda kumaliza matatizo yote

 

 

 

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*