Wavuvi waandaliwe kama jeshi la akiba

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeshauri wavuvi wote waandaliwe kama Jeshi la Akiba la Uokozi kama ilivyo kwa Mgambo kwenye Jeshi la Nchi Kavu.

Kauli imetolewa leo tarehe 9 Novemba 2022 na Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu ajali ya ndege ya Kampuni ya Precision iliyotokea tarehe 6 Novemba 2022.

‘‘Kutokana na kazi ya uokoaji inayofanywa na wavuvi, TEF tunapendekeza wavuvi wote sasa waandaliwe kama Jeshi la Akiba la Uokozi kama ilivyo kwa Mgambo kwenye Jeshi la Nchi Kavu.

Balile amesema, TEF imepokea kwa masikitiko vifo vya watu 19 waliokufa katika ajali hiyo ‘‘TEF inatoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, pia tunawaombea wote walioumia wapone haraka.’’

Amesema, matukio ya ajali yakiwamo hii ya ndege ya Precision, meli ya MV Bukoba, MV Spice Islander na nyingine zilizotokea majini, kimsingi zimepoteza maisha ya watu wengi kwa sababu ya uzembe na ukosefu wa vifaa vya uokoaji.

‘‘TEF inatambua na kupongeza kazi kubwa ya uokoaji iliyofanywa na wavuvi wadogo katika ajali ya Precision. Hii si mara ya kwanza kwa wavuvi kufanya kazi ya kishujaa ya uokoaji kama hii. Walifanya hivyo wakati wa MV Bukoba, MV Spice Islander na katika ajali nyingine ndogo ndogo za majini,’’ amesema.

Amesema, wakati tukiendelea na maombolezo, tunaisihi serikali ifanye uwekezaji mkubwa katika mafunzo na vifaa vya uokoaji zikiwamo helikopta, kwani hakuna mwenye uhakika kuwa ajali ya Precision majini ndiyo itakuwa ya mwisho.

 

 

 

 

 

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*