Wanahabari wawaangukia wabunge muswada wa habari

WADAU wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), wameanza harakati za kukutana na wabunge, jijini Dodoma kwa lengo la kufafanua umuhimu wa kujumuisha vipengele vya sheria ya habari kabla ya kujalidiliwa muswada wa habari.

Muswada huo uliowasilishwa bungeni tarehe 10 Februari 2023, ambapo unatarajiwa kujadiliwa kwenye bunge la sasa la bajeti lile la Septemba mwaka huu.

Miongoni wa wadau hao kutoka CoRI ni pamoja na Deus Kibamba; Saumu Mwalimu, Ofisa Programu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT); Neville Meena, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN).

Deus Kibamba, Mjumbe wa CoRI amesema, sababu kubwa ni kuhakikisha wabunge wanaelewa zaidi dhamira ya wanahabari na uhuru wa habari nchini.

“Bado tuna imani wabunge watatuelewa, tumekuja kukutana nao ili tueleze zaidi, kwa nini baadhi ya vifungu vilivyoachwa nje ni muhimu kuingia kwenye muswada,” amesema.

James Marenga, MISA TAN amesema, wabunge ndio watunga sheria, na muswada umeishafikishwa kwao hivyo ni muhimu tukakutana nao.

“Tulianza na serikali na wakatusikiliza, wakawasilisha kile walichowasilisha bungeni. Ni wakati sasa na sisi kukutana na wabunge kwa ufafanuzi zaidi, naamini wabunge ni waelewa na watatuelewa,” amesema Marenga ambaye ni wakili wa kujitegemea.

Neville Meena kutoka TEF amesema, kinachofanywa na CoRI (kukutana na wabunge) ni jambo la kawaida pale kunapokuwa na hatua za utungwaji wa sheria.

“Ni suala la kawaida pale panapokuwepo na hatua za utungwaji wa sheria, taasisi husika ikawa inatoa ufafanuzi zaidi juu ya kile inachopigania.

“Tumeona ni fursa kwetu sasa kukutana na wabunge ili kuwaeleza nini tunapigania na kwa nini. Nafasi hii tunapaswa kuitumia vizuri na ndio maana tupo hapa Dodoma,” amesema.

Akizungumza kwenye mkutano wa wadau hao uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 20 Februari 2023, Deodatus Balile TEF alisema, ni muhimu kwa CoRI kukutana na wabunge ili kushawishi baadhi ya vipengele ‘vilivyotelekezwa’ kwenye muswada huo.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*