Wanahabari wajadili makali Sheria ya Makosa ya Mtandaoni

WADAU wa habari nchini, wamependekeza kuwepo kwa mabadiliko makubwa katika Sheria ya Makosa ya Mtandaoni kutokana na kujikita zaidi kwenye dhana.
Kauli hiyo ilitolewa kwenye mkutano wa wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali nchini uliosimamiwa na Jukwaa kwa Wahariri Tanzania (TEF), uliofanyika tarehe 9 Juni 2022 jijini Dar es Salaam.
“Waandishi wanaweza kuweka shinikizo, Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ikafanyiwa marekebisho upya. Vifungu vingi vinajiekeza kwenye dhana, na ni ngumu kuhakiki dhana mahakamani,” James Marenga, wakili wa kujitegemea akitoa mada katika mkutano.

Marenga alitoa kauli hiyo akimuunga mkono Imma Mbuguni, Mhariri wa Majira aliyesema, kwa namna sheria hiyo ilivyopitishwa, haikupata muda wa kutosha kujadiliwa na kuonwa madhara yake.
“Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ifutwe na mchakato wake uanze upya. Sheria hii pamoja na uzito wake, kwanza ilipitishwa kwa hati ya dharura lakini vifungu vyake vingi vinajikita katika dhana,” alisema Mbuguni.
Kwenye mkutano huo, Wakili Marenga alieleza kuwa, iwapo wanahabari wataamua kwa pamoja kuhakikisha sheria hiyo inapitiwa upya, inawezekana.
“Mchakato wake una safari lakini inawezekana, sheri hii katika ukweli wake inaleta tabu sana mahakamani, kwenye kesi zote mahakama imekuwa ikishindwa kwa kuwa, ni vigumu kwa mahakama kuhakiki dhana ya mwandishi. Sheria imezama kwenye dhana pekee,” alisema Wakili Marenga.
Joseph Mwendapole kutoka Nipashe alisema, changamoto kubwa ya Sheria ya Makosa ya Mtandaoni imejielekeza katika kuwatia woga waandishi.
“Katika sheria hii, vifungu vyake vingi vinajielekeza katika kutisha waandishi, ndio maana utaona unalazimishwa kutaja chanzo cha taarifa ama mchangiaji katika mtandao, kupekua waandishi ofisini kwao na mengine mengi,” alisema Mwendapole.
Wakili Marenga alisema, Sheria hiyo kifungu 38-42 kinatoa nguvu iliyopitiliza kwa polisi kufanya ukaguzi bila amri ya mahakama.
“Mahakama inapaswa kuwa ndio pekee yenye kutoa kibali cha ukaguzi, ile habari ya polisi kwenda moja kwa moja, hapana.
Alisema, maeneo mengine yenye ukakasi kwenye sheria hiyo ni pamoja na kifungu kinachoruhusu kesi kuendelea na hata kufikiwa hukumu bila muhusika kuwepo.
Wakili huyo ameeleza, kuwepo kwa kifungu hiki kunaweza mwanahabari kukamatwa kokote aliko bila kujua shauri lake lilivyoendeshwa.
“Unaweza kuwa barabarani kwenye kazi zako, ukashtukia umekamatwa bila kujua, sasa kifungu cha namna hii ni hatari katika majukumu ya mwanahabari,” alisema Wakili Marenga.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*