
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Nevile Meena amesema, waandishi wa habari wana wigo mpana wa kufikisha taarifa zao na kuifanya jamii ichukue hatua au ishinikize hatua zichukuliwe kulingana na kile walichokisoma, kukisikia au kukiona.
Meena ametoa kauli hiyo leo tarehe 22 Oktoba 2022 wakati akizungumzia umuhimu wa wanahabari kuchochea maendeleo, uzalishaji mali na mabadiliko ya sheria kwenye warsha ya kuwajengea uwezo wahariri kuandika na kupitia habari za uchechemuzi wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari.
“Leo hii mitandao ya kijamii na katuni zimekuwa zikitumika kufikisha ujumbe kwa jamii na kuleta mabadiliko makubwa, cha msingi ni lazima sheria ziweke misingi imara ya Watanzania kuwa na uhuru wa kujieleza, kupata habari na kusambaza” amesema.
Jabir Idrisa, Mhariri wa Gazeti la MwanHalisi amesema, jamii inapaswa iendelee kupigia kelele kwa kushirikiana na vyombo vya habari juu ya marekebisho ya sheria zinazokwaza uhuru wa habari.
“Juzi tu kuna mtu kule Simiyu amefungwa miaka 7 na faini ya Sh15 milioni kwasababu ya kumtukana kiongozi, sheria ya makosa ya mtandao tunayoilalamikia ndiyo imetumika, tuendelee kupigania marekebisho ya sheria zinazominya haki za binadamu” amesema.
Naye Tumaini Mbibo, amesema watu wanaweza kudhani sheria ni mbaya lakini kumbe hawazijui hivyo jambo la msingi ni kuwawezesha wazijue ili wasizivunje na kuingilia haki za watu wengine
“Hatuwezi kudai mabadiliko ya sheria kama hatuzijui, tufanye uzengezi wa mabadiliko ya sheria tunazozilalamikia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili tupate matokeo chanya” alisema
Be the first to comment