
WAHARIRI wa vyombo vya habari nchini, wamefanya ziara katika Kiwanda cha Kuzalisha Mbolea Asili cha ITRACOM, kilichopo nje kidogo ya Mkoa wa Dodoma.
Ziara hiyo imefanyika leo tarehe 11 Januari 2023, ikiwa ni siku baada ya kukutana na Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo katika mkutano wake uliojumuisha wahariri, maofisa wa Wizara ya Kilimo na wadau wa kilimo.
Ziara hiyo imeratibiwa na Wizara ya Kilimo ikilenga kuonesha hatua mbalimbali zinazochukuliwa na wizara hiyo ili kuongeza tija katika kilimo.
Akizungumza kuhusu kiwanda hicho, Nduwimana Nazaire ambaye ni mkurugenzi wa kiwanda hicho alisema, ITRACOM kinamilikiwa kwa 100% na mwekezaji kutoka Burundi.
Na kwamba, kilianza kujegwa Mwaka 2021 ambapo lengo la awali lilikuwa kuzalisha mbolea asili tani 600,000 kwa mwaka.
‘‘Wakati tunakuja kuanza kujenga, tulikusudia kuzalisha tani 600,000 kwa mwaka lakini baada ya kuanza ujenzi, utafiti wetu ulionesha uwepo wa hitajio zaidi.
‘‘Tuliamua kuongeza ardhi kwa ajili ya kuongeza kiwanda. Kwa sasa kiwanda kimeanza kuzalisha mbolea, tunatarajia kitakamilika mwishoni mwa mwaka 2023 na 2024 tunatarajia kuzalisha mbolea tani 1,000,000, kila mwaka’’ amesema Nazaire.
Amesema, ITRACOM inatarajia kuwa na biashara nzuri nchini na kwamba, lengo la kutosheleza nchi likifikiwa, watauza mbole katika nchi nyingine za Afrika.
Awali Bashe alisema, Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza zaidi kwenye kilimo ili kitatua changamoto za muda mrefu katika sekta hiyo.
“Hatuwezi kutatua shida ile ile kila siku. Serikali imeamua kuwekeza zaidi katika kilimo ili kilete tija katika uchumi,” alisema.
Be the first to comment