
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imeeleza sababu ya kupungua kwa fedha za nje hususani Dola ya Marekani (USD) nchini, kwamba ni kutokana na nchi hiyo kuongeza riba kwenye soko lake.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi BoT, Dk. Suleiman Misango akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini leo tarehe 6 Juni 2023, amesema Marekani ilichukua hatua hiyo ili kuvutia wawekezaji sambamba na kuimarisha soko lake.
Amewaeleza wahariri kuwa, Marekani ilichukua mkondo huo kutokana na kuongezeka mfumuko wa bei uliosababishwa na Vrusi vya Korona (Uviko-19), Mabadiliko Tabia Nchi na Vita ya Ukrain.
“Kutokana na changamoto ya Uviko-19, Mabadiliko Tabia Nchi na Vita ya Ukrain katika uchumi wa dunia, benki ziliamua kubadilisha mwelekeo wa sera ya fedha kwa kupandisha riba.
“Baada ya kuyumba kwa uchumi, Marekani iliamua kuongeza kiwango cha riba kwenye soko lake.
“Ongezeko hilo limechochea uwekezaji katika soko lake na kusababisha upungufu katika soko la nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania,” amesema.
Ameeleza, kuanzia mwaka 2022 mpaka sasa, mwenendo wa uchumi wa dunia sio wa kuridhisha kutokana na Uviko-19, Mabadiliko Tabia Nchi pamoja na Vita inayoendelea nchini Ukraine.
Amesema, Urusi na Ukrain ni sehemu muhimu ya uzalishaji wa bidhaa zinazotumika kwa wingi duniani na hivyo kusababisha athari kubwa.
“Urusi na Ukrain wanazalisha robo tatu ya ngano inayozalishwa duniani. Urusi ni ya pili kwa kuzalisha gesi asilia duniani, pia ni ya tatu katika uzalishaji mafuta na inazalisha 6% ya makaa ya mawe dunia.
“Ukrain inazalisha kiwango kikubwa cha mafuta ya kula na mahindi. Unaweza kuona ni kwa namna gani vita hiyo imechangia tatizo la uchimu,” amesema.
Hata hivyo amesema, Dola za Marekani zinatarajiwa kuongezeka katika kipindi cha Julai na Septemba kutokana na matarajio ya ongezeko la watalii nchini.
Be the first to comment