
WADAU wa Umoja wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) wameeleza kuwa, Muswada wa Mabadiliko ys Sheria ya Huduma za Habari uliowasilishwa bungeni tarehe 10 Februari 2023, haujabeba hata nusu ya mapendekezo ya wadau wa habari nchini.
Akizunguza katika Kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa na ITV, tarehe 24 Machi 2023, Deous Kibamba ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo alisema, kwenye muswada huo sehemu kubwa ya makubaliano kati yao na serikali hayamo.
“Yapo mambo ambayo tulikubaliana na serikali yaingie kwenye kwenye muswada wa sheria ya habari, lakini hayakuingizwa. Kwa uchache, muswada huu uliowasilishwa bungeni, usingepungua vifungu 16 tulivyojaliliana.
“Mimi maeneo yaliyorekebishwa hapa yapo matatu tu. Kuna maeneo mawili yamerekebishwa halafu kote kunapunguza tu adhabu na wala hakurekebishi, kwa mimi tungeweza kusema ni muswada wa kupunguza adhabu.
Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) alisema, baadhi ya maofisa wa serikali ndio wamekuwa kikwazo kikubwa kuelekea sheria ya habari inayotarajiwa.
“Sasa hivi tunazungumza wapo watu wachache ambao hawaelewi na wanadhani wao ndio wameshika ithibati ya mawasiliani katika nchini hii, hata yale mliokubaliana mwisho wanakwenda kuacha nusu yake.
“Ndio maana mnaona tunasema, hata baadhi ya yale tuliyokubaliana, hayakuwekwa kwenye muswada.
Balile alisema, baadhi ya maeneo ambayo serikali na wadau walikubaliana kufanyiwa marekebisho lakini hayakugushwa na muswada ni pamoja na mamlaka ya Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO) kubaki na nguvu ya kufungia magazeti.
“Kifungu cha 9 tulitaka Mkurugenzi wa Habari aondolewe mamlaka ya kutoa leseni. Awe na mamlaka ya kusajili kama ilivyokuwa awali, ikiwa hivyo hatokaa akaamka asubuhi akasitsha leseni lakini haiko hivyo kwenye muswada huu.
“Tulisema vimeundwa vyombo vingi ndani ya sheria hiyo na tulikubaliana kiundwe chombo kimoja cha kusimamia tasnia hiyo, lakini bado haikubadilishwa kama tulivyokubaliana,” alisema.
James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari, Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA TAN) alisema, idadi ya marekebisho ya vifungu ndani ya muswada wa habari haifiki hata nusu ya yale waliyokubaliana na serikali.
“Vifungu tuliyofanyia marekebisho vilikuwa 20 lakini yaliyowekwa kwenye muswada hayafiki nusu,” alisema.
Dk. Rose Reuben, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) alisema, alitarajia muswada huu uwe kwa maslahi ya wanahabari, walahabari na nchi kwa ujumla.
“Tumefanya kazi kwa muda mrefu, tulikubaliana kifungu kwa kifungu. Hata vile tulivyokubaliana kwamba, havijakaa katika kuleta utendaji mzuri wa kazi, bado vimerudi vile vile.
“Ingekuwa vizuri sheria hii ikafanyiwa marekebisho peke yake, kuichanganya itapunguza umuhimu wake. Wabunge wanapoijadili ikiwa yenyewe, ni rahisi kwenda kifungu kwa kifungu na kutoa maoni ambayo ni ya kina,” alisema Dk. Rose.
Be the first to comment