Wadau waanza kuchakata Muswada Sheria wa Habari

WADAU wa habari nchini, wameanza kukutana ili kuchakata Mapendekezo ya Muswada wa Madiliko ya Sheria ya Huduma za Habari nchini.

Wakati leo tarehe 13 Machi 2023, Baraza la Habari Tanzania (MCT), likikutana na wadau wengine kuchakata muswada huo, Umoja wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), wanatarajia kukutana Jumanne wiki hii mjini Bagamoyo.

Muswada huo uliwasilishwa bungeni tarehe 10 Februari 2023, ambapo sasa wadau wa habari wanakutana ili kupitia vipengele mbalimbali vilivyowasilishwa na serikali.

Akizungumzia vikao hivyo vya uchambuzi wa muswada, James Marenga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN) amesema, ni jukumu la wadau kupitia vipengele hivyo.

“Serikali imeishatoa mapendekezo, sasa ni jukumu letu kuangalia vifungu tulivyokuwa tunataka vibadilishwe, vimefanyiwa kazi?

“Kama bado, tunatakiwa kupeleka mapendekezo kwa kamati husika ili muswada ukirejeshwa bungeni, wabunge wawe na mapendekezo yaliyoshiba,” alisema Marenga ambaye ni wakili wa kujitegemea.

Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) alisema, kuna uwezekano wa kupata sheria nzuri ya habari kama wadau watakuwa pamoja na kushirikiana.

“Sheria ikiwa nzuri kila mmoja wetu atafurahi, kila sekta itakuwa. Bado tuna nafasi ya kujadili kwa kina Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari,” alisema Balile.

Hivi karibuni, katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na ITV, Nape Nnauye ambaye ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari alisema, wadau wa habari nchi bado wana fursa ya kuendelea kutoa maoni yao.

“Waandishi wa habari na wadau wengine wa tasnia hiyo, bado wanayo nafasi ya kutoa maoni yao juu ya muswada wa habari uliowasilishwa bungeni tarehe 10 Februari 2023,” alisema Nape.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*