
SHERIA za habari nchini haziwezi kubaki kama zilivyo wakati dunia inakwenda mbele.
Kauli hiyo ilitolewa na Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), tarehe 8 Novemba 2022 wakati akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma.
TEF na CoRI walikutana na mbunge huyo kuzungumzia baadhi ya vipengele vilivyopo kwenye sheria ya habari ya mwaka 2016 vinavyokandamiza uhuru wa habari nchini.
‘‘Mimi na wabunge wenzangu tutashirikiana. Dunia imebadilika na hatuwezi kubaki hapa tulipo,’ alisema Jerry na kuongeza ‘‘nitazungumza na (wabunge) wenzange na kisha tutaona namna ya kufanya.’’
Kikao hicho nje ya viwanja vya bunge, kiliongozwa na Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF ambpo alimweleza Jerry kwamba, sheria ya habari ya mwaka 2016 imeweka mazingira makubwa ya kumuhofisha mwandishi wa habari.
Balile alisema, baadhi ya vipengele vya sheria ya mwaka 2016 vinaua tasnia ya habari akitolea mfano, kipengele kinachompa nguvu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kufungia chombo cha habari kwa namna anavyoona inafaa.
‘‘Katika safari ya mabadiliko haya, tumeungana taasisi zote za habari ili kuwa na kauli moja. Tumeunganisha nguvu ili kufikia lengo,’’ alisema Balile.
James Marenga, Mjumbe wa CoRI kutoka Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA-TAN) alimweleza Jerry kwamba, tasnia ya habari haina tofauti na tasnia nyingine nchini katika utendaji kazi.
Marenga amabaye ni wakili wa kujitegemea alihoji, ikiwa mawakili wanatengeneza taratibu zao na kuzifanya kuwa rejea katika kazi zao, inashindikanaje wanahabari kujiwekea utaratibu wa ‘kujihukumu’ kama ilivyo tasnia nyingine?
‘‘Mimi ni mwanasheria, katika taasisi yetu tulitengeneza cord of conduct wenyewe na hizo ndio zinatuongoza, ni busara kwa wanahabari nao kuwa na utaratibu wao kisheria unaosimamiwa na wenyewe katika kuhakikisha maadili ya uandishi wa habari yanafuatwa,’’ alisema.
Jessy Kwayu, Mkurugenzi Mkuu wa Media Brains Inc Ltd alisema, sheria ya habari ya mwaka 2016 ilipitishwa katika mazingira ambayo si rafiki.
‘‘Vipengele 19 vya sheria hiyo vilijaribiwa kwenye sheria za nchi, vikaonekana kutoingia katika mizani ya kisheria,’’ alisema Kwayu.
Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA alisema, kwa mazingira ya sasa, waandishi wanashindwa kuandika habari kwa uhuru.
‘‘Kutokana na sheria zetu kubana waandishi, sasa vyombo vya habari ndio vinaripoti taarifa zetu tena kwa namna watakavyo,’’ alisema.
Be the first to comment