Wadau wa habari, serikali wazungumza lugha moja

WAKATI serikali ikieleza nia yake ya kuhakikisha muafaka unapatikana katika Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Habari, wadau wa habari wamekiri kuwepo kwa nia hiyo.

James Marenga, Wakili wa Kujitegemea na mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), amesema nia ya serikali katika kupata muafaka wa vipengele vya Sheria ya Habari vyenye ukakasi inaonekana wazi.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 27 Agosti 2022, wakati akizungumza katika Kipindi cha Jicho Letu Ndani ya Habari kinachorushwa na Televisheni ya Star (Star TV).

‘‘Katika hili la Mchakato wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari, sisi wadau wa habari tunaiona nia ya serikali katika kufanikisha hili. Serikali hii imepokea na kukubali kufanyia kazi vipengele mbalimbali, tunakwenda vizuri,’’ amesema Wakili Marenga.

Wakili Marenga amesema, wadau wa habari wamekuwa wakilenga vifungu vinavyotisha waandishi na uhai wa tasnia ya habari nchini na kwamba, sio sheria yote ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 hazifai.

“Kabla ya kuwapo kwa sheria hiyo, kulikuwa na sheria ya mwaka 2006 ambayo ilikuwa na changamoto kubwa sana ya udhibiti na uchapishaji.

“Sheria hiyo ilikuwa ikimpa mamlaka makubwa sana Waziri wa Habari kudhibiti uchapishaji wa magazeti,” amesema Marenga.

Na kwamba, mamlaka hayo kwa waziri, sheria mpya ilipotungwa (Sheria ya Huduma za Habari ya 2016) ikayahamisha na kuyapeleka kwa wenda Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ambapo sasa anaweza kufunga magazeti, kunyima leseni wanahabari na hata kutoa hukumu kwa vyombo vya habari.

Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF alisema, Serikali ya Awamu ya Sita inaonesha utofauti katika kusikiliza na kushughulikia Mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya Habari.

‘‘Kuna tofauti kati ya serikali iliyopita nah ii ya Awamu ya Sita katika kusimamia suala hili, sasa hivi serikali inasikiliza na imeitisha mkutano na wadau katika kushughulikia suala hili,’’ amesema.

Wakati wadau hao wakisema hivyo, Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amenukuliwa akisema kuwa, ni wakati Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo akapunguziwa mamlaka.

Nape alitoa kauli hiyo tarehe 24 Agosti 2022, wakati akizungumza na Mtangazaji Regina Mziwanda katika Kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Alisema, si jambo linalokubalika kwa mtu mmoja kuwa mlalamikaji katika kesi, msikilizaji katika kesi hiyo hiyo na mwisho akatoa hukumu, akisisitiza hukumu hiyo haowezi kuwa sawa.

“Duniani kote ukitaka haki itendeke, ni muhimu anayelalamika, anayetengeneza mashitaka na anayekwenda kusikiliza mashitaka wawe ni watu tofauti ili haki itendeke,” alisema.

 

 

 

 

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*