
WADAU wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), wamewaomba wabunge kuwasikiliza na kuwaelewa katika harakati zao za kuongeza vipengele vilivyoachwa kwenye Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari uliowasilishwa bungeni tarehe 10 Februari 2023.
Akizungumza kwenye mkutano wa CoRI, leo tarehe 20 Aprili 2023 jijini Dar es Salaam, Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amesema, bado safari ya kuhakikisha tasnia ya habari inapata sheria chanya inaendelea.
“Tutakwenda kuzungumza na wabunge kuhusu athari zinazoweza kuifika tasnia ya habari, kutokana na baadhi ya vifungu vilivyomo kwenye sheria na marekebisho yaliyofanywa na serikali ili watusaidie kurekebisha siku wakianza kujadili bungeni,” amesema.
Nevile Meena, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF, ameishukuru serikali kutokana na lengo la kuifanya tasnia ya habari kuwa huru hasa kusimamia mchakato wa mabadiliko ya sheria ya tasnia hiyo.
Meena amesema, pamoja na kile kilichowasilishwa bungeni katika Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari, bado kuna vipengele muhimu vya sheria hiyo vimeachwa nje.
“Kusudio jema la serikali tumeliona. Limefanya kile ilichofanya kwa lengo lilelile la kuboresa mazingira ya habari na wanahabari, tunashukuru katika hilo maana baadhi tumeyaona kwenye muswada.
“Lakini sheria ikibaki kama ilivyopendekezwa kwenye muswada ule, hatuwezi kufanya kazi kwa uhuru na weledi tuliokusudia. Hatususi kwa kile kilichopelekwa, tutaendelea kushawishi kuda mabadiliko ten ana tena. Mchakato wa sheria ni wa kuendelea, tukitoka sisi watakuja wengine kuendeleza tulipoishia,” amesema Meena.
Deus Kibamba, Mjumbe wa CoRI amesema, serikali imeipa heshima tasnia ya habari kwa kuanzisha na kusimamia mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari mpaka hapa ulipo.
Na kwamba, serikali ilikusudia kuondoa vikwazo na ndio maana Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari una mambo mazuri ndani yake.
“Muswada huu ambao serikali imeupeleka bungeni, una mambo mazuri lakini ni machache, mengi bado hayaingizwa. Tunaomba wabunge wajue kuwa kuna mambo mengine zaidi ya habari ambayo tumependekeza, tunaomba yaingie kwa lengo lile lile la kuimarisha tasnia ya habari,” amesema.
James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Misa-Tan ambaye pia ni wakili wa kujitegemea mesema, sheria ina upungufu ambao unapaswa upigiwe kelele na ufanyiwe marekebisho ili sekta ya habari ikue zaidi.
Amesema, mapendekezo ya sheria yaliyotolewa na serikali ni maeneo tisa tu kati ya 21 yaliyopendekezwa yafanyiwe marekebisho na Serikali.
Na kwamba, miongoni mwa mapendekezo yaliyofanyiwa kazi na Serikali na wanaunga mkono kifungu cha 5 (1) kwa kumuondoa Mkurugenzi wa Habari Maelezo kuwa mratibu wa matangazo kwa vyombo vya habari.
“Kifungu 38 kinachozungumzia kashfa ambavyo awali ilionekana ni jinai nacho kimefanyiwa marekebisho lakini mengi ni kupunguzwa kwa makosa na adhabu zake badala ya kuondoa” amesema.
Rose Mwalongo, kutoka Taasisi ya Vyombo vya Vyombo kwa Maendeleo ya Jamii (TAMCOTE) amesema, angetamani kuona mapendekezo ya wadau wa habari yote yameingizwa kwenye Muswada wa Sheria ya Habari yuliwasilishwa bungeni.
“Kama mwanahabari nilitamani kuona mapendekezo yote yamepelekwa na kuwa kwenye muswada wa sheria, lakini mengi hayapo. Kuna hili la magazeti kuendelea kukata leseni kila mwaka, hili naamini linapaswa kuondolewa,” amesema.
Be the first to comment