Wabunge: Tutaishauri kamati muswada wa habari

BAADHI ya wabunge wameeleza kusudio la kuishauri kamati ya bunge itakayokabidhiwa Muswada wa Habari ili kuboresha mapendekezo zaidi.

Kauli hiyo imetolewa na wabunge tofauti walipokutana na timu ya Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma.

Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo (CCM), mkoani Tanga ameahidi kushirikiana na wadau wa habari kuhakikisha tasnia hiyo inakuwa na sheria bora.

Katika mazungumzo yake na wadau hao, Shangazi ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria, alieleza ukakasi uliopo kwa baadhi ya vipengele vya sheria vilivyomo kwenye muswada huo uliwasilishwa bungeni tarehe 10 Februari 2023.

Akigusia hoja ya Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kuhusu kuwekwa ukomo wa chini wa adhabu, Shangazi alisema jambo hilo hata mahakimu linawapa tabu.

“Tuliwahi kukutana na mahakama ambapo mahakimu tuliwaeleza watuambie baadhi ya changamoto wanazozipata katika utendaji kazi wao.

“Moja ya changamoto walilyoeleza ni sheria kuwawekewa ukomo wa chini wa adhabu, jambo hilo wanasema linawapa tabu sana,” alisema.

Kauli hiyo ilitanguliwa na ya Balile aliposema, sio kila kisa la mwandishi linastahili kifungo kama ambavyo sheria inaelekeza.

Balile alisema, awali sheria ilikuwa inaelekeza kifungo kisichopungua miaka mitano na baada ya vikao na serikali, muswada uliowasilishwa bungeni umepunguza na kuweka miaka mitatu.

“Sio kila kosa kwa mwanahabari linahitaji kifungo, makosa yanatofautiana, wakati mwingine kosa linaweza kuhitaji mtu kupewa adhabu ya mwezi mmoja ama kifungo cha nje.

“Hii inategemea na uzito wa kosa, lakini sheria ilivyowekwa, inamlazimisha jaji kutoa kifungo kisichopungua miaka mitatu hata kama kosa ni dogo linalohitaji onyo,” alisema Balile.

Salome Makamba, Mbunge wa Viti Maalum alisema, asilimia 35 ya mapendekezo ya wadau wa habari yaliyopitishwa ni machache, walau yangevuka asilimia 50 ama 60.

Na kwamba, kuna kila sababu ya kuishauri kamati kujumuisha mapendekezo yaliyoachwa kadiri itavyowezekana ingawa sio rahisi kubeba yote.

“Nimejifunza zaidi kutoka kwenu lakini kuna jambo tunapaswa kufanya ili kuwa na sheria bora. Tutaishauri vizuri kamati pale tutapokutana ili kuangalia yale yaliyoachwa nje na umuhimu wa kuyajumuisha kwenye muswada,” alisema Salome.

Mbunge Justin Ngamoha, Mbunge wa Kilolo akizungumza na James Marenga kutoka MISA TAN na Deus Kibamba ambaye ni mjumbe wa CoRI alisema, ni muhimu sana kuangalia marekebisho ya sheria hiyo.

Mbunge huyo alisema, eneo la habari ni muhimu kwa jamii na nchi hivyo, inahitaji uangalizi wa kutunga sheria zitazowezesha uhuru ambao utaisaidia jamii na serikali.

“Najua eneo la habari lina umuhimu mkubwa kwa nchi, sheria zake zinapaswa kutoa nafasi katika utendaji uliotukuka. Tutaangalia na kuishauri kamati namna bora ya kuwa na sheria zenye uahi mrefu kwenye tasnia ya habari,” alisema.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*