
OUSMANE Niang, Naibu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, Tawi la Tanzania (UNICEF – Tanzania), ameshauri kuongezwa kasi ya kampeni ya kuzuia mabinti chini ya umri wa miaka 18 kuolewa.
Niang alitoa kauli hiyo wakati wa utoaji tuzo kwa waandishi wa habari za watoto waliofanya vizuri kwa mwaka 2022. Tuzo hizo zilitolewa tarehe 29 Desemba 2022, jijini Dar es Salaam kwa ushirikiano wa UNICEF na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
‘‘Tuzuie mabinti wenye umri mdogo kuolewa, binti asiolewe kabla ya kuwa na umri wa miaka 18. Tuendelee kushirikiana na TEF katika kampeni hii,” alisema.
Katika tuzo hizo, Faraja Masinde kutoka Mtanzania Digital, alikuwa mshindi wa jumla katika orodha ya washindi hao.
Washindi wengine ni Tumaini Msowoya (Mwananchi & Shamba FM), Marco Maduhu (Nipashe), Aidan Mhando (Chanel Ten), Anord Kairembo (Radio Kwizera), Vick Kimaro (Habari Leo), Jurieth Mkireri (Nipashe), Judith Ndibalema (Majira), Shua Ndereka (Mviwata Radio), Sabina Martine (CHAI FM – Mbeya), Anna Sombida (EATV) na Stansaus Lambet (Dar 24).
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa TEF aliwata Wahariri na wanahabari kuungana katika kuhakikisha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayotoa fursa kwa binti chini ya umri wa miaka 18 kuolewa, inabadilishwa.
Pia aliwataka wanahabari kutoingia hofu katika kuripoti matukio mbalimbali yanayohusu watoto.
‘‘Najua huwa kuna vitisho kama yule aliyetishiwa kupelekwa mahakamani lakini msihofu,’ alisema Balile.
Neville Meena, mratibu wa tuzo hizo alisema, aliwataka waandishi hao kuongeza juhudi na umahiri kwa kufuatilia kwa karibu taarifa za zinazohusu watoto.
Be the first to comment