
AFISA Muhifadhi Wakimbizi Mwandamizi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), nchini Tanzania Boniface Kinyanjui ameshauri serikali iweke mazingira mazuri ya kuruhusu wakimbizi kuzalisha mali ama kutoa huduma katika jamii kwa kuwa, wapo wenye ujuzi.
Kinyanjui ametoa kauli hiyo mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2022, wakati akizungumza kwenye warsha na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) iliyolenga kuzungumzia wajibu wa serikali na UNHCR pia haki za wakimbizi waliopo nchini.
‘‘Wakimbizi na wale wanaoomba hifadhi sio watu wanaopendwa sana katika nchi nyingi. Sisi tungependa kuona wakimbizi wakipewa nafasi ya kujimudu kimaisha katika uzalishaji mali maana ni wanadamu kama wengine.
‘‘Katika wakimbizi kuna wataalamu wengi ambao wanaweza kusaidia jamii. Mfano; kuna mkimbizi alitoka Sudani Kusini na lipita Tanzania akaenda Afrika Kusini. Huko yeye ndiye aliyetengeneza mfumo wa kutoa maji kwenye mwili kupitia tundu za pua wakati ule wa shida kubwa ya UVIKO-19,’’ amesema.
Pia amesema, Serikali ya Tanzania imefanikiwa kulinda amani yake na kwamba, ni nchi iliyohifadhi wakimbizi kwa muda mrefu tangu Uhuru ikiwa ni miongini mwa nchi chache ambazo ziliruhusu baadhi ya wakimbizi kuwa raia wake.
‘‘Amani haitoki juu kushuka chini, inalindwa na serikali, Serikali ya Tanzania imefanikiwa katika hili.…, Tanzania ni nchi ya amani lakini imezingirwa (na nchi zenye wasiwasi wa amani),’’ amesema.
Be the first to comment