
Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Joyce Shebe amesema, uhuru wa habari nchini kwa kiwango chake umeimarika.
Joyce ametoa kauli hiyo leo tarehe 1 Mei 2023, visiwani Zanzibar wakati akitoa hotuba yake mbele ya wadau mbalimbali wa habari walioshiriki katika ufunguzi wa Kongamano la Wanahabari kuelekea Maadhimisho ya Miaka 30 ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanayotarajiwa kufanyika Mei 03, 2023.
Amefafanua kuwa, kongamano hilo ni muhimu na la kipekee sio tu kwa sekta ya habari bali kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi ikiwa ni siku ya kwanza ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yenye Kaulimbiu “Kuunda Mustakabali wa Haki, Uhuru wa Kujieleza kama Kichocheo cha Haki nyingine Zote za Kibinadamu”.
“Kwa umoja wetu, hatuna budi kutafakari namna ambavyo tunaendelea kuhamasisha kuwepo kwa uhuru wa kujieleza, ikiwa ni miaka 30 tangu kuanzishwa kwa maadhimisho.
“Ni muda muafaka kwetu kutafakari hali ya uhuru wa kujieleza sambamba na hali ya vyombo vya habari nchini ili kupata suluhu ambazo zitasaidia kuchochea katika kuhakikisha jamii inapata fursa ya kujieleza, kutambua haki zake na kuwa na uwezo wa kuzidai haki hizo”, amesema Joyce.
Ametoa rai kwa wanahabari kutumia siku hizo tatu kutafakari na kujadiliana mambo ambayo yatawavusha kutoka walipo na kuelekea kwenye fursa nzuri zaidi ambapo uhuru wa uhariri, kutafuta habari, kuhoji na kujieleza vinakuwa ni suala ambalo kila Mtanzania anapaswa kujivunia.
Amewakumbusha wanahabari kuwa pamoja na kudai uhuru wa vyombo vya habari, wafahamu kwamba hakuna uhuru usio na mipaka, hivyo wanapaswa kuzingatia misingi ya taaluma na maadili pamoja na kujali faragha za watu wakati wakitimiza majukumu yao.
“Tukumbuke kwamba tunalo jukumu la kulinda Utanzania wetu kwa kuandika habari zenye kuhamasisha utamaduni wetu na kuchagiza maendeleo kwa kuzingatia maadili na taaluma”, amesema.
Sheba ametoa shukrani kwa Serikali kwa namna ambavyo wameendelea kushirikiana na Vyombo vya Habari pamoja na wadau mbalimbali ambao wanaunga mkono sekta ya habari.
Be the first to comment