‘Tunatoa adhabu kubwa kukabili bidhaa feki’

Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani (FCC), Dk. Agrey Mlimuka amesema, tume hiyo hutoa adhabu kubwa kwa wanaobainika kuwa na bidhaa bandia/feki ili kukatisha tamaa wanaofanya biashara hizo.

Na kwamba, wanaofanya muunganiko wa bidhaa hizo ni wafanyabiashara wakubwa na wenye pesa.

Dk. Mlimuka ametoa kauli hiyo leo tarehe 13 Aprili 2023, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari.

“Suala la bidhaa feki linahusisha wafanyabiashara wakubwa, huwa tunatoa adhabu kubwa ili kukatisha tamaa.

“Sisi kama tume tuna mamlaka makubwa ya kuchunguza na kutoa adhabu,” amesema Dk. Mlimuka.

Amesema, vita ya bidhaa feki ni kubwa na kwamba, wakati mwingine huweza kuwahusisha hata wanahabari.

“Mnaweza kutumika kwenye vita ya bidhaa feki. Tunaweza kutoa habari lakini madhara yake yakawa makubwa.

“Mtu analeta Televisheni 500 halafu anasema ni kwa matumizi yake mwenyewe, kweli? Unajua huyu anataka kukwepa tu,” amesema.


Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF amesema, semina za taasisi na wahariri zinasaidia kwa kiwango kikubwa kukuza uelewa.

“Kama tutakuwa tunaruhusu ile tabia ya kununua bidhaa halafu muuzaji anasema ukishanunua hairudishwi, tunaweza kutoa nafasi kubwa ya kuwa na bidhaa feki sokoni.

“Lazima anayenunua apewe stakabadhi na pale bidhaa ile ikibainika kuwa ni feki, aruhusiwe kuirudieha,” amesema.

William Urio, Mkurugenzi Mkuu wa FCC amesema, semina hiyo imehusu kuwaongezea uelewa wahariri katika maeneo mawili ambayo ni muunganiko wa kampuni na bidhaa feki.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*