
JAMES Marenga, wakili wa kujitegemea amesema, licha ya serikali kujiandaa kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi za Kimtandao, ingependeza mapendekezo ya wahadau wa habari kuhusu mabadiliko ya sheria za habari yakawasilishwa Bunge hili la Septemba.
Wakili Marenga ametoa kauli hiyo leo tarehe 8 Septemba 2022 ikiwa ni siku moja baada ya serikali kueleza kwamba, imepata kibali cha kupeleka bungeni muswada wa sheria ya ulinzi wa taarifa biafsi za kimtandao.
Kauli ya serikali ilitolewa tarehe 7 Septemba 2022 na Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakati akifungua kongamano la siku mbili lililowakutanisha wadau mbalimbali wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
“Baada ya muswada huu wa washeria kupelekwa bungeni, kila mdau atatakiwa kutoa maoni yake ili kuweza kukamilisha sheria hiyo. Baraza la Mawaziri tumeshaandaa muswada wa sheria hiyo ili kuondoa kabisa tatizo la baadhi ya watu wanaotumia vibaya mitandao.
“Lengo la Serikali halitaki kumwacha nyuma mtanzania kwa kuwa teknolojia ya kisasa itasaidia mambo mengi ikiwemo kwenye ajira na hata kupata wawekezaji wengi,” alisema Nape
Hata hivyo Wakili Marenga alisema, wadau wadau wa habari, wangependa kuona Waziri Nape anatimiza ahadi yake ya kuwasilisha mapendekezo ya wadau kuhusu mabadiliko ya sheria za habari katika bunge la mwezi huu.
“Wadau wangependa kuoana ahadi ya Mh. Waziri Nape ya kupeleka Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari yanafanikiwa kwenye Bunge hili la mwezi Septemba mwaka huu ili mchakato wa mabadiliko hayo ukamilike,” alisema Wakili Marenga.
Alisema, mjadala wa serikali na wadau wa Habari ulihusu Sheria ya Huduma za Habari 2016 na kwamba, kuna baadhi ya vipengele tayari wamekubaliana.
“Mjadala wa serikali na wadau ulihusu Sheria ya Huduma za Habari 2016, na yaliyojadiliwa ni mapendekezo ya wadau na yale ya serikali, kuna vipengele tulikubalia na vingine bado vipo kwenye mjadala,” alisema Marenga.
Akizungumzia sheria ya kulinda taarifa binafsi za kimtandao Wakili Marenga amesema, sheria hiyo si ya wadau wa habari pekee, inahusu watu wote.
“Halafu hii sheria ya data protection (ulinzi wa taarifa binafsi ) sio kwa ajili ya wadau wa habari pekee, ni sheria muhimu kwa watu wote,” alisema.
Be the first to comment