Tumemwambia Nape, tutarudi kwake – Balile

DEODATUS Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amesema, licha ya sehemu ya mapendekezo ya wadau kutoingizwa kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari, bado yaliyomo yanahitajika.

Akizungumza kwenye Kongamano la 12 la Kitaaluma la TEF leo tarehe 30 Machi 2023, mjini Morogoro amesema, wadau wa tasnia wanapaswa kuendelea kushikamana na kuepuka mivutano inayoweza kusababisha kutoeleweka.

“Hivi vifungu (katika muswada wa habari) tukisema tuvikatae mpaka pale vyote vitakapopitishwa, tunaweza kuondoka duniani tukiwa hatujavipata,” amesema.

Amesema, kwenye hotuba yake tarehe 29 Machi 2023 katika kongamano hilo alimweleza Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye alikuwa mgeni rasmi kwamba, asituchoke.

“Tumemwambia waziri (Nape) hapa Pamoja na kazi aliyoifanya kwenye muswada ule, lakini asituchoke maana tutaendelea kumfuata,” amesema.

Amesema, licha ya serikali kubadili baadhi ya vifungu lakini bado kuna vifungu wadau ‘tunapaswa kuendelea kuvidai.’

Akitaja baadhi ya vifungu ‘hatari’ katika tasnia ya habari ambavyo vimeachwa kwenye muswada huo uliosomwa bungeni kwa mara ya kwanza tarehe 10 Februari 2023, ni pamoja na serikali kuwa na mamlaka ya kuagiza habari kuchapwa kwa kigezo cha ‘maslahi ya taifa.’

“Utapolazimisha mwongozo wa stori, je ikiwa na shida nani anawajibika?”

Akizungumzia suala la kashfa kwa maiti amesema, pamoja na kufafanuliwa kwamba, ni suala lisilowezekana bado serikali imeendelea kulibeba.

“Suala la kashfa lazima anayekashifiwa afike mahakamani kueleza kwa namna gani ameumizwa na kashfa hiyo haliwezekani, sasa hapa unawezaje kumpeleka maiti mahakamani akahojiwe?” amehoji.

Amesema, ndani ya muswada huo bado waziri amepewa nafasi ya kuzuia maudhui yanayobishaniwa, na kwamba kipengele hicho kinampa nafasi waziri kuingilia uhuru wa habari.

Pia Balile amesema, suala la ukomo wa chini wa adhabu kwa ‘mtuhumiwa’ mwanahabari pale anapofanya kosa linapaswa kuwa mikononi mwa hakimu.

“Mwanzoni hakukuwa na ukomo wa mwisho (juu) wa adhabu, tukapambana ukawekwa, lakini kuna ukomo wa chini ambapo hakimu anapaswa kumfunga si chini ya miaka mitatu.

“Tunasema sio kila kosa linahitaji kifungo, kuna makosa mengine yanahitaji kuonywa ama kifungo cha nje ama adhabu ya mwezi mmoja, kuweka ukomo wa miaka mitatu, ni kumlazimisha hakimu adhabu hiyo hata kama ko sani dogo,” amesema.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*