‘TEF inaamini katika diplomasia’

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema, katika harakati za kupigania marekebisho ya sheria rafiki kwa vyombo vya habari, TEF inaamini katika njia za kidiplomasia.

Balile ametoa kauli hiyo kwenye mkutano wa mtandaoni (online meeting) tarehe 27 Aprili 2023, akijibu swali la mhariri kutoka Sahara Media, Michael Noel aliyetaka kujua, iwapo mapendekezo yaliyotolewa na wadau wa habari na kuachwa, ni hatua gani wanahabari watachukua.

“Ikiwa sehemu kubwa ya mapendekezo yetu yataendelea kuachwa, ni hatua gani zaidi tunaweza kuchukua ikiwa ni pamoja na maandamano ili kushinikiza?” ameuliza.

Balile amesema, Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) walikutana na baadhi ya wabunge kwa ajili ya kuwaeleza umuhimu wa kujumuisha vipengele vilivyoachwa kwenye muswada wa habari, uliosomwa bungeni kwa mara ya kwanza tarehe 10 Februari 2023, na kwamba yapo mafanikio.

“Tunaona kabisa kwamba kuna mabadiliko, lakini sisi kama TEF hoja ya kutumia nguvu hatujaifikiria na siyo sehemu ya mipango yetu, tunaamini katika diplomasia,” amesema Balile.

Kwenye mkutano huo, James Marenga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa MISA TAN amesema, bado kuna changamoto inayohitaji kufanyiwa kazi.

Na kwamba, baadhi ya wabunge wanaelewa changamoto za vyombo vya habari hasa kupitia sheria iliyopo na wengine hawazifahamu kwa undani.

“Bado tunachangamoto sana ya kupata upimaji halisi, kwani kuna baadhi ya wabunge ambao wanaunga mkono hiki tunachokilalamikia juu ya kuwasilishwa bungeni kwa muswada wa habari ambao una mapungufu akiwamo.

“Miongoni mwa wanaounga mkono moja kwa moja ni Mbunge wa Viti Maalum, Salome Makamba ambaye alitaka kushikilia shilingi ya Waziri kwa serikali kupeleka sehemu ndogo ya muswada wa marekebisho ya sheria ya habari,” amesema.

Rashidi Kejo, mhariri kutoka Gazeti la Mwananchi ameshauri kutengenezwa vipande vipande vya sheria ilivyopendekezwa na vilivyopitishwa na kuvisambaza kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya ufahamu zaidi.

Jessy Kwayu kutoka Jarida la FAMA amesema, mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari hauishi kwa mara moja, ametaka kujua ni kwa asilimia ngapi harakati hizi zimefanikiwa mpaka sasa?

Hata hivyo mto mada, James Marenga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa MISA TAN amesema, bado kuna changamoto ya kupata uhalisia kwa kuwa, baadhi waliokutana nao walionesha kuelewa na baadhi bado, na kwamba mwenedo mpaka sasa ni mzuri.

Peter Nyanje amewapongeza wajumbe wa CoRI kwa kiwango walichofikia kwenye mchakato wa Mabdiliko ya Sheria ya Habari na kuwataka wanahabari kuandika kwa ukubwa zaidi.

“Suala hili ni la kwetu lakini namna tunavyolichukuliwa si kwa umuhimu unaostahili, vyombo vya habari viandike kwa kiwango kikubwa kuhusu suala hili,” amesema.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*