‘Sheria ya Uhalifu Mtandaoni inaminya uhuru wa habari’

KUTUNGWA kwa Sheria ya Uhalifu wa Mtandaoni Mwaka 2015, kumeweka mazingira ya wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari vya mtandaoni katika hatari kubwa. Sheria hii imekuja kuminya uhuru wa habari na si kuimarisha.

Kauli hiyo imetolewa na James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA – TAN) katika mafunzo ya waandishi wa habari za mtandanoni yaliyoandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) leo tarehe 20 Julai 2022, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye semina hiyo Marenga ambaye ni wakili wa kujitegemea amesema “tusipokuwa makini, sheria hizi zitaumiza wengi.”

“Neno kama ‘kwa namna nyingine ama kusudio na kinyume cha sheria,’ ni maneno hatari yanayotumika hasa kuharamisha jambo ambalo sio kosa kisheria. Maneno haya unaweza kuyaona ya kawaida, lakini ni hatari sana,” amesema Wakili Marenga.

Kwenye semina na wanahabari hao, Wakili Marenga amesema, kwenye sheria hiyo kuna adhabu zilizowekwa kwa makosa ambayo hayapo wazi kinyume na Ibara ya 13 (6)(C) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia amesema, sheria hiyo kupitia Kifungu 7 (i)(g) iliyotungwa mwaka 2015, imevuruga uhuru wa faragha ambapo taarifa binafsi za mtu zinaweza kuchukuliwa na polisi kinyume na Ibara ya 16(i) ya Katiba ya Tanzania.

“Sheria hii katika Kifungu cha 50(2)(b) kinaondoa haki ya mtu kukata rufaa kinyume na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, lakini pia Kifungu cha 38(2)(b) cha sheria hii kinaruhusu usikilizwaji wa shauri mahakamani hata bila muhusika kuwepo,” amesema Marenga.

Akizungumza kwenye semina hiyo, Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa TEF, amesema kuna tatizo kwenye sheria hiyo na kwamba, baadhi ya vipengele vinapaswa kuondolewa kabisa.

‘’Sheria inaruhusu kesi yako kuendeshwa bila wewe mwenywe kujua. Kesi unaweza kufunguliwa Mwanza, siku unashuka mtaani unakutwa unapigwa tanganyikajeki.

“Wanaweza kufanya hivyo, sheria inaruhusu. Tunapopigania hii sheria iondolewe ama ipitiwe upya, watu wajue tunapigania maslahi ya wengi,’’ amesema Balile.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*