Serikali yaandaa mikakati kukabiliana na mabadiliko tabianchi

Serikali imesema, imeandaa hatua na mikakati madhubuti yenye kuibua fursa za miradi ya kijamii kwa wananchi, ikiwemo kanuni na mwongozo wa biashara ya kaboni ikiwa ni njia mbadala ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 19 Juni 2023 na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Hassan Mitawi wakati akifunga warsha ya siku moja baina ya wahariri na menejimenti ya ofisi hiyo, iliyolenga kujenga uelewa kuhusu kanuni na mwongozo wa biashara ya kaboni.

Mitawi amesema, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoathiriwa na athatri za mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika hali inayojidhihirisha kupitia matukio ya mvua zisizotabirika, ongezeko la joto, ukame na mafuriko, ambapo athari hizo zimeathiri sekta za kijamii na kiuchumi.

“Pamoja na changamoto zinazochangiwa na mabadiliko ya tabia nchi kumekuwa na fursa na jitihada mbalimbali ambazo zimechukuliwa na serikali ikiwa ni pamoja na mapitio ya sera, uandaaji wa kanuni, mikakati na miongozo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi – Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Hassan Mitawi.

Mitawi amesema biashara ya kaboni ni miongoni mwa nyenzo muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani inayotekelezwa na nchi wanachama wa Maktaba wa Mabadiliko ya tabianchi, itifaki ya Kyoto na makubaliano ya Paris, ambapo Tanzania ni  mwanachama wa mikataba hiyo.

Kwa mujibu wa Mitawi, pamoja na kuwepo kwa sera na mikakati mbalimbali, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa kanuni na mwongozo wa usimamizi wa biashara ya kaboni ya mwaka 2022 ili kuweka utaratibu na masharti yanayopaswa kuzingatiwa na  wadau na wawekezaji wa biashara hiyo nchini.

“Kanuni na mwongozo wa biashara ya kaboni tayari zilishatangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 636 la tarehe 28 Oktoba, 2022 na hivyo kuwa tayari kwa matumizi.

“Nyenzo hizi zimejikita katika kuimarisha mchango wa nchi katika jitihada za kupunguza uzalishaji wa gesi joto” amesema Mitawi.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*