Serikali: Tumepokea maoni ya wadau wa habari

NAPE Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amewahakikishia wadau wa habari kwamba, serikali itakamilisha mchakato wa mabadiliko ya vipengele vya sheria ya habari.

Kwenye kikao chake na wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), tarehe 21 Novemba 2022, jijini Dar es Salaam Nape alisema, serikali imepokea maoni yao kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari Na 12 ya 2016.

” Niwahakikishie kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inayo nia ya dhati katika jambo hili. Nimekuja mwenyewe kuwasilikiliza na imani yangu ni kuona sekta inaendelea kukua” amesema.

Kikao hicho cha pili cha Wadau wa Kupata Habari (CoRI) na serikali cha kupitia mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari, kiliongozwa na Nape mwenyewe.

“…tupo kwa ajili ya kufanya mapitio ya mwisho ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016,” alisema Nape.

Nje ya kikao hicho, Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), alisema una muelekeo mzuri kuelekea mabadiliko ya sheria ya habari.

‘‘Kikao kilikuwa kizuri, serikali imeendelea kuonesha dhamira yake ambayo ilikuwa nayo tangu mwanzo. Tumemaliza na serikali inaendelea na hatua zake kabla ya kupelekwa bungeni.

‘‘Suala la mabadiliko ya vipengele vya sheria lina mchakato wake, cha msingi serikali imetoa fursa, na si kutoa peke yake, inaendelea kuchukua hatua,’’ alisema Balile.

Miongoni mwa mapendekezo ya CoRI kwa serikali ni pamoja na mamlaka haya ya Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO) yafutwe na kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine, kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.

Wadau wanataka marekebisho dhidi ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni badala ya usajili wa moja kwa moja.

Pia wadau hao wanapendekeza magazeti yasiendeshwe kwa kupewa leseni, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti changamoto ya ufutwaji holela  wa leseni na kuvutia wawekezaji.

Miongoni mwa wadau walioshiriki kikao nicho ni TEF, Umoja wa  Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Chama wa Waandishi wa Habari Tanzania (JOWUTA) na MISA- Tanzania.

 

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*