‘Serikali imekuwa wazi mabadiliko ya sheria habari’

DEOGRATIUS Nsokolo, Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari amesema, serikali imekuwa wazi katika mchakato wa mabadiliko sheria ya habari.

Nsokolo alitoa kauli hiyo leo wakati akitoa maoni yake na kwamba, maendeleo ya mchakato huo yanatokana na kuridhiwa na Serikali ya Rais Samia.

“Rais Samia tangu alipoungia madarakani, alikuwa karibu na sekta ya habari na kutoa matumaini ya kufanyiwa marejeo kwa sheria hi ya mwaka 2016. Na tayari matokeo yake ni wadau wa habari na serikali kukaa kwa pamoja na kuainisha vipengele gani tungependa viondolewe,” alisema.

Nsokolo alisema, utayari huo umeoneshwa wazi hasa baada ya wasaidizi wa Rais Samia kuonesha kwa vitendo pia hatua kwa hatua kwa kukutana na wadau wa tasnia hiyo kwenye vikao vya pamoja.

“Upande wa serikali na wadau umeishamaliza kazi yake ya kuainisha vipengele hivyo, kilichotarajiwa ni mwaka huu mwezi wa tisa mapendekezo hayo kupelekwa bungeni lakini kwa bahati mbaya haikuwezekana.

“Serikali kwa uwazi kabisa ilieleza sababu ya mkwamo kwamba, Waziri (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) alisema, mapendekezo hayo hayakufikishwa bungeni kwa kuwa, kuna hatua zilikuwa hazijakamilika. Hii ni dhamira ya wazi kabisa ya serikali hii,” alisema.

Alisema, kazi iliyobaki sasa ni upande wa serikali kukamilisha mchakato na kisha mapendekezo hayo kupelekwa bungeni kwa mujibu wa sheria za nchini.

“Wito wangu, mchakato huo uende kwa kasi ile ile kwa sababu, mabadiliko hayo yatawezesha waandishi wa habari kuwa huru zaidi, pia kufanya kazi zao kwa weledi.

“Mambo hayo yanayokwaza uhuru wa habari yakiondolewa, itasaidia sana kwani  habari ni muhimu kwa maendeleo ya nchi,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, alisema mchakato huu unakwenda kwa kuwa, rais aliyepo madarakani ana dhamira njema na sekta ya habari.

Na kwamba, baada ya wadau wa habari kufanya vikao serikali, wadau wanasubiri matunda ya vikao hivyo kwa kupelekwa mapendekezo ya wadau wa habari bungeni.

“Katika mchakato huu, tumekuwa tukishiriki kuzungumza na waziri husika ili tukubaliane katika sehemu mbalimbali ya vifungu vya sheria ya habari,” alisema Balile na kuongeza:

“Tulifanya mkutano wa mwisho mwezi Novemba ambao tulisema, sasa huu uwe mkutano wa mwisho ili sheria ya huduma za habari ipelekwe bungeni.”

Hivi karibuni, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa alisema serikali inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya vipengele vya Sheria ya Huduma za Habari ili wabunge wakiridhia utekelezaji wake ufanyike.

“Kwa sasa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya sheria hii ili wabunge wakiridhia, tuendelee na utekelezaji wake,” alisema Msigwa.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*