
NAPE Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amesema, serikali inakusudia vyombo vya habari vifanye kazi kwa uhuru na kwamba, haitaviingilia kwenye uhuru wao.
“Serikali itasimamia na kulinda uhuru wa kujieleza. Itahakikisha inafanya kila linalowezekana kulinda haki hiyo,” alisema Nape kwenye ziara yake katika Kampuni ya Mwananchi Communication inayomiliki vyombo vya habari vya Mwananchi, The Citizen na MwanaSpoti.
Waziri Nape amesema, Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari yaliowasilishwa bungeni taarehe 10 Februari 2023, yanalenga kuimarisha uhuru wa kujieleza nchini.
Pia amesema, serikali inataka kuwa mlezi wa uhuru wa kujieleza “serikali haitaki kuingilia biashara ya vyombo vya habari. Inachotaka ni kuwa mlezi wa uhuru wa kujieleza na tunataka wamiliki wa vyombo vya habari, waendeshe biashara zao kama ilivyo kwa tasnia nyingine kama wanasheria, madaktari na wengine.”
Nape amesema, wakati ilipotungwa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016, kulikuwa na vilio vingi.
“Tusingeweza kuendelea na vilio hivyo, hivyo tumependekeza baadhi ya mabadiliko kwenye sheria hiyo,” amesema.
Na kwamba, muswada huo ukipitishwa kwa taratibu za bunge na kutiwa saini na rais kuwa sheria kamili, utasaidia kuleta mageuzi makubwa kwenye tasnia ya habari nchini.
Amesema, baada ya muswada kusomwa bungeni, sasa utakabidhiwa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ambapo itakuwa na jukumu la kuwaita tena wadau wa masuala ya habari kwa ajili ya kuwasikiliza, kisha kamati hiyo ya bunge itapeleka maoni ya wadau bungeni kabla ya Bunge kuanza kujadili maoni ya serikali kuhusu sheria hiyo.
“Tulifanya mazungumzo ya kutosha kwa mwaka mzima kati ya serikali na wadau juu ya maboresho ya ile sheria, na yale tuliyokubaliana, tumeyazingatia kama serikali kwenye mapendekezo yetu bungeni,” amesema Nape.
Bakari Machumu, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) amesema, mchakato kuelekea sheria hiyo, umekuwa wa majadiliano zaidi kati ya serikali na wadau waha habari.
“Kuna mapendekezo ambayo tuliyapeleka, yamesomwa. Kwa hiyo, tunachoangalia kwa sasa ni kwenda mbele kujua nini kimewekwa na kitajadiliwa kwa njia ipi” amesema Machumu.
Be the first to comment