Sera ya Habari itakuwa moja – Nape

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema, miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kutekelezwa katika bajeti ya wizara hiyo ya mwaka 2023/2024 ni kuwa na sera moja inayosimamia habari na utangazaji.

Nape ametoa kauli hiyo leo tarehe 19 Mei 2023, bungeni wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.

“Tunakusudia kufanya mapitio ya Sera ya Habari na Utangazaji ili kuendana na mabadiliko katika sekta ya habari, na hapa tunakusudia tuwe na sheria moja inayosimamia sekta ya habari kwa ujumla,” amesema Nape.

Na kwamba, wizara itahamasisha vyombo vya habari vya ndani na nje kutangaza Tanzania, sambamba na kuendelea kujenga na kufunga miundombinu ya utangazaji katika wilaya tisa za Tanzania.

Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya amemtaka Nape kusaidia wanahabari kuwa na mikataba inayoeleweka kwani baadhi yao wanaendelea kuumizwa na wamiliki.

“Asilimia 90 ya waandishi wa habari hawalipwi, hasa wa taasisi binafsi. Nape kuna vyombo vya habari miaka 10 hawalipwi lakini wanakosa mtetezi.

“Uandishi sio kazi ya kujitolea, ni kazi kama udaktari, ualimu. Nini hatma yao hawa waandishi? Katika hili, mimi nitashika shilingi yak oleo,” amesema Bulaya.

Akizungumzia laini za simu zilizosajiliwa, Nape amesema kuna ongezeko ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2022.

“Takwimu zinaonesha laini za simu zilizosajiliwa nchini zimeongezeka kutoka milioni 55.7 mwezi Aprili 2022 hadi kufikia milioni 62.3 mwezi Aprili 2023, sawa na ongezeko la asilimia 11.8,” amesema.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ni miongoni wahariri wa jukwaa hilo waliofika bungeni kushuhudia uwasilishwaji wa bajeti ya wizara hiyo.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*