Rais Samia anataka msiwe waoga – Nape

NAPE Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amesema, Rais Samia Suluhu Hassan anataka wanahabari wafanye kazi yao bila woga, upendeleo na uonevu.

Akizungumza kwenye Kongamano la 12 la Kitaaluma la Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Nape amesema, Rais Samia, Serikali na Wanahabari wenyewe wapo tayari kuhakikisha wanafikia mabadiliko ya Sheria ya Habari, hivyo hakuna kitakachokwamisha.

“Rais Samia anawasalimia sana, ameniambia, kazungumze nao waambie wafanye kazi kitaaluma bila woga, bila upendeleo wala uonevu, haya ni maneno yake mwenyewe,” amesema Nape.

Amesema kuwa, kutokana na umuhimu wa kongamano hilo, Rais Samia amemruhusu kuhudhuria ingawa kuna ujio wa Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris na kwamba, Waziri mwenzake ambaye alitaka kuhudhuria kongamano hilo, hakuruhusiwa.

“Kuna shughuli nyingine ya kumkaribisha Makamu wa Rais wa Marekani, lakini nilipomwomba rais kuhudhuria kongamano hili, aliniruhusu, mwenzangu hakuruhusiwa.

Nape amesema, Rais Samia ni muumini wa haki ya kujieleza na kutoa maoni, hivyo haoni sababu ya kuminya uhuru wa habari.

“Rais alishawahi kuniambia wakati wa mchakato ya kupitia Sheria ya Habari kuwa, tuhakikishe hatuingilii haki ya watu kujieleza.

“Nasi tumekuwa tukilifanya hilo, niwaombe kwa pamoja tutafsiri maono ya rais wetu, yeye nia na dhamira yake ni kuona uhuru wa habari unaleta tija kwa nchi,” amesema.

Katika mkutano huo, Nape alipewa tuzo ya heshima ikiwa ni tuzo ya kwanza ya kupewa Waziri wa Habari tangu nchi hii kupata Uhuru.

Nape alikabidhiwa tuzo hiyo na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile.

Hata hivyo, Balile amesifu Nape kwa ushirikiano wake wa karibu katika safari ya mabadiliko ya Sheria ya Habari na anaamini miaka miwili ijayo Tanzania itashika nafasi ya 50 kwa kuwa na uhuru wa habari kutoka nafasi ya 120 ya sasa.

Balile amesema kuwa tangu Rais Samia ameingia madarakani, amebadili upepo wa tasnia ya habari na hivi sasa uhuru upo tofauti na miaka sita iliyopita.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*