Rais Mwinyi: Tunaheshimu uhuru wa habari

DAKTARI Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibari amesema, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zinaheshimu uhuru wa habari.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 3 Mei 2023, katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ambapo kitaifa yamefanyika visiwani Zanzibar.

“Maadhimisho haya ni muhimu katika kuibua changamoto za kisera, pamoja na kuangalia namna bora ya uboreshaji wa mazingira ya uendeshaji wa vyombo vya habari katika nchi.

“Kwa hakika, serikali zetu zote mbili zinathamini na kuheshimu sana Uhuru wa Vyombo vya Habari. Uhuru huo umeendelea kukua siku hadi siku kwa pande zote mbili za Tanzania,” amesema.

Amesema, Serikali ya Zanzibar tayari imeandaa muswada wa sheria ya habari utaofuta utaratibu wa usajili wa magazeti pamoja na vipengele vingine.

“Kuhusu sheria ya habari kwa upande wa Zanzibar, serikali tayari imeishaandaa muswada wa sheria ambao madhumuni yake ni kufuta sheria iliyopo ya usajili wa magazeti, wakala wa habari na vitabu No.5 ya mwaka 1988… na kutunga sheria mpya ya huduma za habari,” amesema.

Rais Mwinyi amesema, lengo la maadhimisho hayo ni kulinda uhuru wa vyombo vya habari duniani, ambapo serikali zinapata nafsi ya kukutana na wadau wote kwa madhumuni ya kujadiliana uhusiano na mwingiliano wa mabadiliko ya utendaji kazi, usawa wa kijinsia ndani na nje ya vyombo vya habari pia uslama wa waandishi.

Akisoma Azimio la Wanahabari walioshiriki maadhimisho hayo, Joyce Shebe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) amesema, waandishi wamedhamiria kutetea na kulinda uhuru wa habari.

“Tumeadhimia kuhamsisha, kutetea, kuimarisha na kulinda haki ya uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari kama msingi muhimu wa kuimarisha haki zingine za binadamu zinazochangia kwa pamoja kuongeza uelewa wa wananchi, kuhusu haki hizo na ushiriki wao katika shughuliza maendeleo,” amesema.

Shebe ambaye ni Mhariri kutoka Clouds Media amesema, jukumu lingine la wanahabari ni kutetea maslahi ya nchi kwanza kuliko kitu kingine.

“Wanahabari watahakikisha wanatetea na kulinda maslahi ya nchi katika kukuza uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu kuliko kutanguliza maslahi ya wafadhili,” amesema.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*