‘Nilipofungia Gazeti la Uhuru, Raia Mwema nilijisikia vibaya’

Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa amesema katika maisha yake ya uandishi wa habari, siku aliyojisikia vibaya zaidi ni aliyofungia gazeti la Rais Mwema na Uhuru.

Msigwa ametoa kauli hiyo leo ikiwa ni siku ya pili baada ya jana kufunguliwa Kongamano la Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Dunia visiwani Zanzibar, ambapo kilele chake ni tarehe 3 Mei 2023.

Gazeti la Raia Mwema lilifungwa kwa siku 30 kuanzia Septemba 5, 2021 kwa madai ya kukiuka maadili ikiwa ni siku 14 baada ya Gazeti la Uhuru kufungwa.

Akieleza kadhia hiyo kwenye kongamano hilo Msigwa alisema “kati ya siku niliyojisikia vibaya kwenye maisha yangu ya uandishi, ni siku niliyofungia Gazeti la Raia mwema na Uhuru.”

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema tasnia ya habari inahitaji sheria zitakazosimama katikati kwa wanahabari na serikali.

“Tubadilishe sheria si kwa kupendelea waandishi ila kwa heshima ya nchi. Kwenye mabadiliko ya sheria ya habari, tunaamini zaidi kwenye majadiliano kuliko mapambano,” amesema Balile.

Mwenyekiti Mstaafu wa wa TEF, Abasalom Kibanda amewaeleza wajumbe wa kongamano hilo kwamba, wanahabari wanadai sheria ili kuandika habari kwa uhuru na si uholela.

“Tunapodai Uhuru wa Habari, hatudai uholela wa habari bali uhuru wa habari ambao unaenda sambamba na haki na wajibu,” amesema.

Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaa, Prof. Chris Peter Maina amesema kama sheria nzuri haitaandikwa, nia njema ya serikali haitoshi kuipa ulinzi tasnia ya habari.

“Mnaweza kuwa na serikali nzuri yenye nia njema lakini bila sheria hakuna ulinzi kamili wa uhuru wa habari,” amesema Prof Maina.

Hata hivyo, amewashauri waandishi visiwani humo kutumia fursa ya kukutana na Rais Hussein Mwinyi kila mwisho wa mwezi katika kusukuma ajenda ya kubadilisha sheria ya habari, Zanzibar.

Kongamano hilo lilifunguliwa tarehe 1 Mei 2023 na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita.

Waziri huyo aliwataka wanahabari kufuatia habari kwa uhakika ili wananchi waweze kupata taarifa sahihi na kwa wakati.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*