NBS: Sensa 2022 ni ya kidigitali

SENSA ya Watu na Makazi ya mwaka huu, itatumia zaidi vifaa vya kidigitali ili kupata takwimu sahihi.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini katika semina ya siku mbili iliyofanyika mkoani Morogoro, Saidi Amri, Afisa Habari Mwandamizi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), amesema mfumo huo utazuia upikaji wa takwimu kwa mkusanya taarifa (karani).

“Tutatumia zaidi Vishikwambi (tablets) 250,000 ambazo watagawiwa wakusanya takwimu, hizi zitakuwa na ramani itayomuonesha yupo katika kaya ipi na katoka kaya ipi.

“Hata akiruka kaya, itakuwa inaonesha. Karani atapita kaya 70 mpaka 75. Matumizi ya Vishikwambi yalifanyika Ghana, Kenya na hata Afrika Kusini na yalikuwa na matokeo mazuri,” amesema Said.

Amesema, Sensa hufanyika ili serikali iweze kujua takwimu rasmi za watu wake na vitu kwa lengo la kupanga kutoa huduma.

“Kumshawishi mtu kutohesabiwa wakati wa Sensa ya Watu na Makazi ni kosa kisheria,” amesema.

Said amesema, Sensa itaanza  usiku wa tarehe 22 kuamkia tarehe 23 Agosti 2022, ambapo siku hiyo itakuwa mapumziko.

Deogratius Malamsha, Mtaalamu wa Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), amewaeleza wahariri hao kuwa, ipo tabia kwa baadhi ya wananchi kuficha wenye ulemavu na wazee vikongwe.

“Wakati wa sensa sio jambo sahihi kuficha watu wenye ulemvu na wazee. Mkiwaficha mtakuwa hamuwatendei haki.

“Lakini pia mtasababisha serikali kushindwa kuwajua na hata kuwaweka kwenye mpango mzuri wa kuwapatia mahitaji yao,” amesema Malamsha.

Semina hiyo ililenga kuwajengea uwezo wahariri ili waweze kushiriki katika uelimishaji na uhamasishaji wa Sensa.

Baadhi ya mada zilizowasilishwa katika mafunzo hayo ni  umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi na Maandalizi yake, Vyanzo vya Uripoti kwenye Sensa, Mbinu za Uripoti na Mambo ya Kuzingatia na Matumizi ya Mitandao ya Kijamii katika kufanikisha Sensa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*