Nape: Tupo tayari

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema, serikali ipo tayari kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari.

Akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma tarehe 9 Novemba 2022 alisema, serikali haijakaa kimya kuhusu mabadiliko hayo na kwamba, kuna taratibu zinaendelea.

Nape alisema, serikali ilitarajia kupeleka mapendekeo hayo bungeni katika Bunge la Novemba mwaka huu, lakini kwa kuwa taratibu hazikukamilika, haikufanya hivyo kwa kuepuka mivutani kutoka kwa wadau wa habari.

Kwenye kikao hicho na CoRI, Waziri Nape alisema serikali ipo tayari kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari kwa watunga sheria, baada ya kikao cha wadau wa habari na serikali kitakachofanyika tarehe 22 Novemba 2022, jijini Dar es Salaam.

‘‘Serikali tupo tayari kupeleka mabadiliko ya sheri ya habari bungeni baada ya kikao cha mwisho. Baada ya kikao hicho tutakubaliana tuliyokubaliana na ndio yataenda,’’ alisema Nape.

Alisema, haikuwa vyema kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari bungeni wakati kuna maeneo wadau wa habari na serikali walikuwa hawajakubaliana.

‘‘Sisi kama serikali hatujakaa kimya, bado tupo vizuri kwenye mchakato huu. Nia ya serikali mpaka sasa bado ni njema.

‘‘Isingefaa kwenda na mabadishano bungeni. Mpaka sasa kuna maeneo ambayo bado hatujakubaliana na kikao hicho cha mwisho ndio kitatoa mwelekeo wa mapendekezo yote.

Kwenye kikao hicho Nape alisema, uhuru uliopo sasa unapaswa kutumika vizuri.

‘‘Sisi kama tupo happy (tunafuraha) na mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari unavyokwenda, lakini pamoja na yote haya, ni vizuri uhuru uliopo tukautumia vizuri,’’ alisema.

Na kwamba, pamoja na mchakato wa mabadiliko ya sheria kuwa njiani kukamilika, serikali inaangalia pia uhalisia wa mabadiliko hayo ya sheria na mazingira ya sasa.

‘‘Hata kama kuna mapitio tunayofanya, lakini lazima tuangalie uhalisia wa nchini,’’ alisema Nape.

Akizungumzia takwa la Rais Samia Suluhu Hassan la kukutana na wanahabari alilolitoa wakati wa Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD), jijini Arusha Nape alisema, wizara ipo mbioni kuandaa mazingira ya Rais Samia kukutana na wanahabari hao.

‘‘Katika Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Rais aliagiza wizara kutaka kukutana na wanahabari. Tunafanyia kazi hilo,’’ alisema Nape.

Gerson Msigwa, Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), alishauri wanahabari kubaki Pamoja kwenye mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari.

‘‘Tutumie vizuri kipindi hiki ambacho serikali imekuwa tayari kusikiliza. Tubaki Pamoja mpaka mwisho,’’alisema Msigwa.

Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF aliomba wadau wa habari kushiriki vema katika kikao cha mwisho cha serikali na wadau wa habari kwa kuwa ni muhimu.

‘‘Kama kuna mtu anawazo, alilete kupitia umoja wa haki ya kupata habari ili kwenye kikao hicho tuwe na lugha moja,’’ alisema.

Dk. Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) alisema, wadau wa habari wanapaswa kutoa mawazo yao ili ifike mahali wakubaliane katika utungaji wa sheria.

‘‘Tunapaswa kutoa mawazo yetu lakini ili tufike mahali ambapo tunaweza kukubaliani ili kuufanya huu mchakato wa mabadiliko ya sheria uende haraka. Sheria itakapoanza kufanya kazi, tutaanza kuona mabadiliko katika uandishi wa habari ambao ni wakitaaluma,’’ alisema.

James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), alisema katika kikao cha pili, hakuna jambo litalobaki bila kushughulikiwa.

‘‘Baada ya kikao cha pili kama ambavyo imeelezwa na serikali, tunaamini mabadiliko yatakayopelekwa bungeni yatakidhi matakwa ya wanahabari kwa ajili ya kunufaishi wananchi, serikali na tasnia kwa ujumla,’’ alisema.

 

 

 

 

 

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*