
NAPE Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ameungana na wadau wa habari nchini kwa kutaka madaraka ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo yapunguzwe.
“Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo tunataka madaraka yake yapunguzwe,” amesema Nape wakati akizungumza na Salim Kikeke, Mtangazaji wa BBC Swahili – Dira ya Dunia, jijini Dar es Salaam tarehe 24 Agosti 2022.
“Duniani kote ukitaka haki itendeke, ni muhimu anayelalamika, anayetengeneza mashitaka na anayekwenda kusikiliza mashitaka wawe ni watu tofauti ili haki itendeke,” amesema.
Akizungumzia msingi wa utungwaji wa sheria iliyopo sasa (Sheria ya Mwaka 2016), ameeleza lengo ilikuwa kupunguza mikono ya serikali katika kusimamia vyombo vya habari.
Na kwamba, sehemu kubwa ya usimamizi wa vyombo hivyo, ibaki kwa wanataaluma wenyewe tofauti na Sheria ya Habari ya Mwaka 1976 ambayo iliingiza mikono mingi katika kusimamia vyombo vya habari.
“Tulipotunga sheria ya mwaka 2016, lengo lake ilikuwa ni kwamba tupunguze mikono ya serikali katika kuendesha vyombo vya habari. Sheria ya mwaka 1976 ilikuwa imeweka mikono mingi sana.
“Sheria hii tukatamani ipunguze, na namna ya kupunguza ilikuwa ni pamoja na kuunda Baraza Huru la Wanahabari ili yale ya kitaaluma wayamalize huko,” amesema Nape.
Amesema, serikali iliamini kwamba ikipita njia hiyo, itakuwa imefanikiwa kupunguza madaraka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo aliyopewa na sheria ya mwaka 1976.
“Waandishi wa habari kama wanataaluma zingine wakiwemo wanasheria wajisimamie wenyewe, na inawezekana. Sisi kama serikali tubaki na vitu vichache sana vinavyolinda nchi, usalama na afya ya jamii,” amesema.
Be the first to comment