
Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliao na Teknolojia ya Habari amesema, serikali haitapeleka Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Habari bungeni, mpaka wakubaliane na wadau.
Nape ametoa kauli hiyo leo tarehe 26 Agosti 2022, wakati akizungumza na Mtangazaji Regina Mziwanda katika Kipindi cha Idhaa ya Kiswahili kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
BBC iliwaalika Nape na Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kuzungumzia mwenendo wa mabadiliko ya Sheria ya Habari nchini.
‘‘Niwahakikishie wanahabari kwamba, hatutakwenda bungeni bila ya kukubaliana. Hatutaki kutunga sheria halafu kesho tubadilishe, serikali ipo tayari kuondoa baadhi ya vifungu,’’ amesema Nape.
Pia waziri huyo ameshauri uwekezaji kwenye vyombo vya habari uongezwe kwa kuwa, habari za uchunguzi zimeporomoka.
“Tanzania imeporomoka katika habari za uchunguzi,’’ na kwamba, nchi hii kwa miaka mingi ilikuwa na rekodi nzuri katika uhuru wa vyombo vya habari, lakini hapo nyuma kidogo iliyumba.
Amesema, katika kila utawala (jambo likitaka kufanyika) lazima kuwe na utashi wa kisiasa kama ilivyo sasa hivyo, nia ya serikali si kudhibiti vyombo vya habari, bali kutengeneza mazingira mazuri.
Kwenye mjadala huo, Balile amesema serikali ya sasa imetoa fursa tofauti na serikali iliyopita ‘‘hapo awali hata fursa hii ya kuzungumza (Mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya Habari) haikuwepo.’’
Amesema, awali mchakato huo ulianza kwa kasi, hapo katikati ulilega na sasa nguvu ya kwenda mbele imeongezeka na kuwa, kuridhishwa na mwenyendo uliopo.
‘‘Nia ya vyombo vya habari ni kutumikia wananchi. Sisi tunajenga nchi yetu, tutashirikiana na serikali. Hatuombi uhuru wa kusema uongo, tunataka uhuru wa kutoa habari,’’ amesema Balile.
Be the first to comment