Muswada Mabadiliko ya Sheria ya Habari ‘kulainishwa’

MUSWADA wa Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari uliowasilishwa bungeni tarehe 10 Februari 2023, utachambuliwa kwa lugha ya Kiswahili ili ueleweke zaidi.

Kauli hiyo ilitolewa na Deus Kibamba, Mhadhiri wa Masuala ya Diplomasia ambaye pia ni Mjumbe wa Umoja wa Wadau wa Kupata Habari (CoRI), wakati akizungumza katika Kipindi cha Kipima Joto cha ITV, mwishoni mwa wiki. Kibamba alikuwa akijibu swali la Isaac Mpayo, mtangazaji wa kipindi hicho alipohoji kwamba, wadau wa habari wanahakikishaje muswada huo unafika na kueleweka kwa wananchi.

“Tutakaporejea kutoka katika kuuchambua, hautakuja katika maneno haya magumu ya Kingereza, utakuja kwa maneno laini ya (Kiswahili).

“Hivi sasa ndio kikosi chetu kinafanya mkakati kiweze kulainisha ili tuweze kutoa hoja katika lugha ya Kiswahili ambayo wananchi wanaweza kuifikia,” alisema Kibamba.

Kibamba ambaye ni mwandishi wa siku nyingi wa makala za uchambuzi alisema, katika kipindi cha nyuma, wananchi na wadau wa habari waliwahi kupendekeza miswada iwe inawasilishwa kwa lugha mbili tofauti (Kiswahili na Kingereza) na sio lugha moja ya Kingereza kama ilivyo sasa.

“Miswada hii wananchi na sisi wadau tumewahi kupendekeza iwe inatoka katika mtindo ambao unaweza kusambaa vizuri kwa wananchi. Kwa mfano, Mama Anna Makinda alipokuwa Spika wa Bunge, bunge liliwahi kuridhia hoja miswada iwasilishwe kwa lugha ya Kingereza na Kiswahili,” alisema.

Hata hivyo alisema, CoRI inao wajibu wa kuhakikisha maudhui ya muswada huo yanawafikia wananchi ikiwa ni pamoja na kuandika habari fupi fupi pia uchambuzi wa makala kwa lugha laini inayoeleweka kwa wananchi.

Katika kipindi hicho, Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), alimsema CoRI imeunda kamati ya watu sita ambao kwa pamoja watapitia kuuchambua Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari uliosomwa bungeni kwa mara ya kwanza.

“Umoja wa Wadau wa Kupata Habari tumekutana, tukaunda kamati ya watu sita ambayo nimo kwenye hiyo kamati kwamba, twende tuuchambue kwa kina ili twende hatua inayofuata.

“Si yote yaliyopita tuliyokuwa tumependekeza, lakini si yote yaliyobaki. Yaani kuna mabadiliko makubwa yaliyotokea. Mfano: wameondoa kashfa kuwa jinai. Sasa hatutaona mtu anasema ‘umemsema vibaya Waziri.’ Nafikiri hili tuwapomngeze serikali,” alisema.

Joyce Shebe ambaye ni Mhariri kutoka Kituo cha Televisheni cha Clouds alisema, kusomwa kwa mara ya kwanza muswada huo bungeni, kunatoa fursa kwa wadau wa habari kuendelea kutoa mawazo yao na kushirikishwa pia.

“Tunarudia tena kusema kwamba, huu si muswada wa wanahabari pekee, ni muswada wa Watanzania wote kwa sababu mwananchi anahitaji taarifa, na sisi ndio tumeshikilia dhamana ya kuwapa taarifa lakini pia serikali naye ni mdau wa habari,” alisema Shebe.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*