Muswada mabadiliko sheria ya habari kuwasilishwa leo

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema, Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari utawasilishwa leo tarehe 10 Februari 2023.

Nape alibainisha hilo jana jijini Dodoma wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mabadiliko ya ratiba za Bunge.

Awali, Gerson Msigwa ambaye ni Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) alisema, muswada huo ungewasilishwa katika Bunge la Aprili kutokana na ufinyu wa muda katika bunge lililoanza mwishoni mwa Januari mwaka huu.

Hata hivyo, baada ya kauli hiyo, siku iliyofuata Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) lilieleza kutofurahishwa na sababu ilizotolewa na serikali kwamba, imeshindwa kuwasilisha muswada huo kutokana na ratiba ya bunge kubana.

Kwenye kikao chake na wanahabari, Nape alisema muswada huo umepata nafasi ya kuwasilishwa leo baada ya kuzungumza na uongozi wa bunge.

Hata hivyo, ameomba wadau wa habari kuendelea kuaminiana na kwamba, mchakato huo ni wa wadau wote wa habari nchini.

Wadau wa sekta ya habari wamekuwa wakishinikiza sheria hiyo ifanyiwe marekebisho makubwa kwa sababu, ina vifungu ambavyo vinakwamisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.

 

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*