
Fulgence Massawe, Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) amesema, wadau wa habari nchini kuna haja ya kuendelea kupaza sauti ili serikali ifanye mabadiliko stahiki.
Kauli hiyo ilitolewa wakati wa mkutano maalumu uliolenga kupitia na kuchambua kesi mbalimbali katika sekta ya habari, ambazo hukumu zake hazijatekelezwa na serikali licha ya kwamba vyombo husika vya habari vilishinda.
“Mara nyingi Mahakama zinatoa hukumu nzuri zinazolinda uhuru wa habari, lakini hukumu hizo hazitekelezwi. Jambo la kufanyika ni kuendelea kupaza sauti kwa sababu mifumo ya utekelezaji wa mashauri kama haya ni kama hayapo. Ni muhimu kuendelea kufanya uchechemuzi ili serikali ifanye marekebisho,” alisema na kuongeza:
“Tumeona wadau wanasikilizwa kwenye kuboresha sheria, kwa mfano sheria hii ya Huduma za Habari, lakini bado hatujaona mwisho wa siku huu uamuzi unatekelezwa ili tufike mwisho na tuone kweli uhuru wa habari umelindwa na timilifu kwa mujibu wa ibara ya 18 ya Katiba yetu.”
Kajubi Mukajanga, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), alisema kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mtu ama taasisi pale anapoishinda serikali, mahakamani inabidi uiandikie kuiomba itekeleze hukumu na kwamba, uzoefu unaonesha serikali huwa haitekelezi uamuzi wa mahakama.
“Tuwe na utaratibu ambao utafanya uamuzi wa mahakama uweze kutekelezwa. Wananchi wanaamini Mahakama ni chombo cha haki na uamuzi wake utatekelezwa. Siyo kitu kizuri uamuzi wa mahakama ukapuuzwa,” amesema Mukajanga.
Be the first to comment