
KATIKA dunia ya sasa, kuna tatizo la uelewa kuhusu taarifa za haki za watoto na changamoto wanazopitia, ikiwemo wale wenye ulemavu.
Kutokana na hilo, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (Unicef), wameendesha warsha kwa wakuu wa Idaya za Uandishi wa Habari kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali nchini kuhusu uandishi wa habari za watoto wenye tija.
Lengo la warsha hiyo ya siku tatu (tarehe 27-29 Agosti 2022) iliyofanyija mijini Morogoro, ni kuunda na kusaidia kuweka mazingira mazuri ya kufundishia, kuripoti na kuwapa ujuzi walimu hao ili waweze kuwaandaa vijana katika uandishi wa habari za watoto wenye tija.
‘‘Pamoja na kwamba habari zinaripotiwa, mchakato wa habari hizo huacha mambo mengi na wakati mwingine habari hizo zinakosa muendelezo.
‘‘Hii ina maana kwamba, vyombo vya habari havihitaji tu kuripoti kwa haki, uaminifu na usahihi juu ya watoto, lakini lazima pia kutoa nafasi kwa maoni na ubunifu wa watoto wakiwemo wenye ulemavu,’’ amesema Dk. Mukiza.
Paulo Mabuga, Mtaalamu wa Vyombo vya Habari kutoka Mwanza amesema, mwongozo kwa walimu wa waandishi unastahili kuandaliwa kwa ustadi kwa kuwa, ndio wanaowaandaa waandishi wa kesho.
‘‘Kwa hakika, hivi karibuni niliangalia chombo kimoja cha habari, namna walivyoripoti habari ya tukio la mtoto mmoja, inasikitisha. Mwandishi alishindwa kupanga picha, kutoa maelezo na mwisho wa taarifa ile haikuwa na ujumbe wenye athari,’’ amesema Mabuga.
Nassoro Ali, Mkuu wa Idara ya Uandishi wa Habari kutoka Chuo Kikuu cha Waislam Morogoro (MUM) amesema, kuna haja ya kuwaandaa wanafunzi kuyakabili mazingira ya uandishi wa habari za watoto na changamoto zao.
Diana Msovu kutoka Chuo Kikuu cha Iringa, Idara ya Undishi wa Habari amesema, kuna kila sababu ya kuimarisha uandishi wa habari za watoto.
‘‘Nchini kwetu bado uandishi wa habari za namna hii upo chini, unapoangalia uwasilishwaji wa taarifa hizi katika nchi nyingine, ndio utabaini utofauti.
‘‘Hili linapaswa kuanzia vyuoni kwa wanafunzi, kila habari ina umuhimu wake, hivyo zote zinapaswa kuandikwa katika uzito unaofanana,’’ amesema.
Neville Meenda, msimamizi wa mafunzo hayo amesema, mafunzo hayo yanalenga kukabiliana na changamoto iliyo sasa katika siku za usoni.
‘‘Warsha hii ni muhimu kwa kuwa, nyinyi ni walimu tena ndio waandaaji wa waandishi, ni vizuri kujengewa uwezo ili Kwenda kuwaandaa vijana namna ya kuandika habari zinazoweza kubadilisha taswira kwa jamii kuhusu watoto,’’ amesema Neville Meena.
Be the first to comment