Dk. Mpango: Hatuwezi kuruhusu hili liendelee

MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango amesema, kuna baadhi ya viongozi kwa maslahi yao binafsi wanachangia katika uharibifu wa mazingira.

Dk. Mpango ametoa kauli hiyo leo tarehe 19 Desemba 2022, Iringa katika Kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi, Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji.

Kongamano hilo limeratibiwa na Kituo cha Wanaharakati Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA), ambapo Dk. Mpango amesema hatokubali hili liendelee.

“Wapo baadhi ya viongozi kwa maslahi binafsi, wanachangia sana kwenye uharibifu wa mazingira.

“Siamini wakulima wetu masikini, wafugaji kwamba ndio wanaoharibu mazingira. Lazima tunusuru mito yetu yote hasa mito ya kimkakati kama Ruaha, viongozi wa namna hii hawatufai,” amesema Dk. Mpango.

Katika kongamano hilo amesema, mwaka 1980 uharibifu wa mazingira ulifanywa kwa asilimia 42; mwaka 1980 asilimia
50 na mwaka 2012 uharibifu ulikuwa kwa asilimia 68.

Kwenye kongamano hilo,Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ameishauri serikali kuchukua hatua ya kuiondoa Ranchi ya Usangu ambayo ipo ndani ya bonde oevu linalolisha maji Mto Ruaha Mkuu sambamba na kujenga tuta eneo la Ngiliamu ili kuunusuru mto na ukame.

“Sisi tunafanya habari za uchunguzi na tumebaini Ranchi ya Usangu inamilikiwa na familia 12, wamo majaji, wamo wabunge, wamo mawaziri na leo nitakukabidhi majina.

“Ranchi hii ilifutwa na GN No. 28 lakini kamati ya mawaziri wanane iliamua kuiacha,” amesema Balile.

Habibu Mchange ambaye ni Mwenyekiti wa MECIRA amesema, leo ni siku ya 130 Mto Ruaha hautiririshi maji.

  • “Leo Mto Ruaha Mkuu umefikisha siku 130 bila kutiririsha maji, na ukienda hifadhini utasikitika kuona viboko wanagombania mchanga na si maji kutokana na uharibifu wa mazingira, amesema Mchange.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*