
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema, taarifa zinazoripotiwa na vyombo vya habari kuhusu ubadhirifu wa rasilimali za umma, hufuatiliwa kwa karibu na taasisi yake.
“Taarifa zenu huwa tunazitumia kupata maeneo hatarishi katika suala la usimamizi wa rasilimali za umma, kisha kuandaa mpangokazi na ukaguzi katika eneo hilo,” alisema CAG Kichere alipokutana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), jijini Dar es Salaam tarehe 28 Mei 2022.
CAG Kichere alikutana na TEF kwa lengo la kufafanua taarifa ya ripoti ya ukaguzi ya 2020/2021, na hatua zinazoendelea kuchukuliwa. Kwenye mkutano huo, alishukuru vyombo vya habari kwa kufanya uchambuzi wa kina wa ripoti yake.
CAG Kichere alisema, serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), inaendelea kuchukua hatua kutokana na ripoti hiyo.
“Takukuru wamekuwa wakiniomba ripoti za maeneo fulani fulani ya nchi. Nimekuwa nikiwapa na wanakwenda kuzifanyia kazi,” alisema CAG Kichere.
Aliwaeleza wahariri kuwa, ripoti yake ilibaini kasoro mbalimbali ikiwa ni pamoja na Sheria ya Manunuzi ya Umma kutoa mwanya wa fedha za umma kufujwa na watendaji wasio waaminifu kupitia ununuzi wa vitu mbalimbali kwa mfumo wa zabuni wanazotangaza.
Alisema, kutokana na kuwepo kwa mianya ya wazi, ameshauri sheria hiyo ifanyiwe marekebisho ili kuondoa changamoto zinazojitokeza mara kwa mara na kusababisha fedha za umma kufujwa.
Mfano wa changamoto hiyo ni manunuzi yaliyofanywa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ambapo ripoti ya CAG ilibaini vifaa vilivyonunuliwa kwa bei kubwa tofauti na bei halisi ya vifaa hivyo.
“Unakuta kitu sokoni kinauzwa Sh1,500 lakini watu wamenunua kwa Sh5,000, unapofuatilia unaona wamekidhi matakwa na wamefuata sheria na taratibu zinazotakiwa. Kuna haja ya kuifanyia marekebisho sheria ya ununuzi ili kunusuru fedha za umma,” alisema.
Katika mkutano huo, CAG Kichere alitoa fursa ya kujibu maswali ya wahariri, ambapo baadhi yao wakiwemo Joseph Kulangwa na Salim Said Salim waliuliza, anajisikiaje mapendekezo ya ripoti zake kutofanyiwa kazi?
Katika majibu yake, CAG Kichere alisema, kila mkaguzi anapenda kuona ripoti, maoni na mapendekezo anayoyatoa yanafanyiwa kazi ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza zisijirudie katika kaguzi zijazo.
CAG Kichere pia alisema, tatizo lingine alilokutana nalo ni baadhi ya fedha za serikali kutumiwa bila kupita katika Mfuko Mkuu (HAZINA), ambao yeye ndiyo anaidhinisha.
“Hili jambo lilionekana sana, inaonekana fedha nyingi ni zile za miradi zinazotoka kwa wafadhili na kwenda moja kwa moja kwenye miradi husika,” alisema.
Alisema, baadhi ya mashirika ya umma yalikuwa yakitoa gawio kwa serikali huku yakipata hasara, na alipokuwa akiuliza kuhusu fedha za gawio, alijibiwa fedha zile ni mchango.
“Gawio haliwezi kutolewa na shirika linalopata hasara, hivyo wale waliosema wametoa gawio ama walikosea au walifanya hivyo kwa makusudi, mimi waliniambia fedha walizotoa sio gawio ni mchango,” alisema.
Akizungumza na kwa niaba TEF, Salim Said Salim alisema, Ofisi ya CAG imefanya jambo jema kuandaa mkutano huo uliowaongezea uelewa wahariri na waandishi, hivyo akataka ushirikiako huo uboreshwe zaidi.
Be the first to comment