
Balozi wa Uholanzi nchini, Wiebe de Boer amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuweka mazingira wezeshi kwa waandishi wa habari kufanya kazi kwa uhuru na weledi unaotakiwa.
Balozi Boer ametoa kauli hiyo alipokutana na viongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), katika ofisi za ubalozi huo, jijini Dar es Salaam ambapo alisema tangu Rais Samia ameingia madarakani kumekuwa na mwelekeo mzuri katika tasnia ya habari.
“Nampongeza rais kwa kufungua milango katika utendaji kazi wa vyombo vya habari Tanzania, vyombo vya habari sasa visiwe vioga katika kutekeleza majukumu yake.
“Rais ameonyesha namna anavyohitaji vyombo hivyo kuwa huru, wanahabari nao watumie nafasi hiyo kuimarisha uhuru wao,” amesema Balozi Boer.
Katika hatua nyingine Balozi Boer huyo alisema, Rais Samia amefanya jambo kubwa kwa kuunganisha umoja hasa kwa kushirikiana na vyama vya upinzani katika mambo mbalimbali.
“Jambo analofanya Rais Samia ni la kupongezwa, hatua ya kushiriki kwenye mikutano ya vyama vya upinzani, inaonesha kwa kiwango kikubwa anataka kuunganisha nchi.
“Hii ni fursa ya kujenga nchi moja na kushirikiana kujenga uchumi imara. Ni vizuri kwa sasa na vyombo vya habari visiogope kufanya kazi na vyama vya upinzani kwa kuwa hata rais kaonyesha kwamba hakuna tatizo,” alisema.
Pia ameipongeza TEF na wadau wa habari kuonyesha mshikamano katika kupigania uhuru wa habari na kwamba, jambo lolote huenda taratibu mpaka linafanikiwa.
Deodatus Balile, Mwenyekti wa TEF amempongeza Balozi Boer kwa nchi yake kuwa karibu na vyombo vya habari Tanzania.
Hata hivyo, amemhakikishia kwamba vyombo vya habari vya Tanzania vinatarajia kuwa na sheria inayokuza tasnia ya habari na si inayoweka vikwazo vinavyoweza kuua kabisa thamani ya tasnia hiyo.
“Tuna imani na mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari, rais na serikali yake alionesha mapema nia ya kuondoa vikwazo katika uhuru wa habari nchini kwetu.
“Ndiyo maana maana baada ya kuingia madarakani alianza kufungulia vyombo vilivyokuwa vimefungwa ambavyo ni MwanaHalisi, Mawio, Raia Mwema na Tanzania Daima pamoja na Televisheni za mtandaoni.
“…lakini hata katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Habari, kuna vikwazo vimeondolewa ikiwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maeleza kupunguziwa mamlaka,” alisema.
Be the first to comment