Aina saba za fidia WCF

MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), unatoa aina saba ya fidia kwa wateja wake ikiwa ni pamoja na gharama kwa anayemuhudumia mgonjwa ama aliyefikwa na janga.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 20 Machi 2023 na Dk. Abdulsalaam Omar, Mkurugenzi wa Tathmin WCF wakati akiwasilisha mada kwenye semina ya siku moja ya mfuko huo na wahariri wa habari mjini Bagamoyo, Pwani.

Amesema, mafao mengine ni huduma ya matibabu, malipo ya ulemavu wa muda, malipo ya ulemavu wa kudumu.

Pia mfuko huo unatoa malipo kwa anayemuhudumia mgonjwa, huduma za ukarabati na ushauri nasaha, malipa kwa wategemezi endapo mfanyakazi atafariki na pia gharama za mazishi.

Akizungumzia kupunguzwa kwa kiwango cha michango WCF, Dk. John Mduma, Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo amesema, kiwango cha wanachama kutoka sekta binafsi kimepunguzwa kutoka asilimia 10 ya awali na kuwa asilimia 0.5.

“Kuna mambo makubwa katika miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo yameyafanywa WCF.

“Sekta binafsi ilikuwa ikichangia asilimia 10 katika mfuko wa fidia, lakini serikali hii ikapunguza mpaka asilimia 0.6 na katika bajeti ya mwaka huu wa fedha unaotekelezwa, imeshusha na kuwa asilimia 0.5,” amesema Dk. Mduma.

Kwenye semina hiyo, mkurugenzi huyo amesema serikali ilipunguza riba kwa zile taasisi ama wachangiaji waliokuwa wakichelewesha michango lengo likiwa ni kuwashawishi kuendelea kuwatolewa wafanyakazi wao.

“Awali ilikuwa ukichelewesha michango, riba yake ilikuwa asilimia 10 kwa mwezi, lakini Serikali ya Rais Samia ikapunguza na kuwa asilimia mbili tu.

“Lakini pia baada ya kupunguza riba hiyo, iliamua kufuta madeni ya riba kwa wachangiaji ambao walikuwa hawajachangia,” amesema.

Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) aishukuru WCF kwa hatua ya kupunguza kiwango cha michango kutoka kwa waajiri.

“Ni jambo jema lililofanywa na WCF, hata kupunguza riba kutoka asilimia 10 hadi mbili ni jambo la kupongezwa, na hili litachangia kwa waajiri kuendelea kulipa michango ya wafanyakazi wao kwenye mfuko wa WCF,” amesema.

Abraham Siyovelwa, Mwanasheria wa WCF amesema, pale mfanyakazi anapopata ajali akiwa kazini, CFW humuhudumia hata kama hajakamilisha michango yote, kisha WCF hutumia sheria kudai michango hiyo kwa mwajiri.

“Hata mfanyakazi akiwa kwenye likizo ya ugonjwa na mwajiri wake akiendelea kumlipa mshahara, sisi WCF tunamrudishia (mwajiri) mshahara wake kwa kuwa jukumu hilo huwa la WCF,” amesema.

Semina hiyo, WCF ililenga kueleza shughuli zake na faida zinazopatikana kwa waajiri kujiunga na mfuko huo ikiwa ni pamoja na kupunguza mzigo kwao (waajiri) pia kuwapa afueni wafanyakazi pale wanapokutwa na majanga.

Tangaza nasi

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*